UONGOZI wa Azam FC umesema kuwa hauko tayari kumuachia winga wake, Mrisho Ngasa kwenda katika timu yoyote na bado wanahitaji huduma yake.
Kumekuwa na taarifa za chini chini za Yanga kutaka kumsajili mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kuichezea klabu hiyo.
Akizungumza Dar es salaam jana, Msemaji wa timu hiyo Jafar Idd Maganga alisema kuwa timu yake haifikirii kumuachia nyota huyo hasa katika kipindi hiki ambacho timu hiyo inakabiliwa na michuano ya kimataifa.
“Habari zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari juu ya mchezaji wetu Ngasa kutaka kuhamia katika timu ya Yanga si za kweli kwani bado ana mkataba na timu yetu na bado tunamhitaji ukizingatia kuwa tunakabiliwa na michuano ya kimataifa.
“Ngasa amekuwa msaada mkubwa sana akishirikiana na wachezaji wengine na kuifanikisha timu kushika nafasi ya pili na sasa tunaiwakilisha nchi michuano ya kombe la shirikisho,kwa hali hiyo haitakuwa rahisi kumuachia,” alisema.
Timu hizo zinamn’gan’gani mchezaji huyo ambaye pia ni tegemeo kwa timu ya Taifa zikiwa na malengo tofauti ya kuviimarisha vikosi vyao.
Azam wanakabiliwa na michuano ya kombe la Kagame yanayotarajiwa kufanyaka hapa nchini lakini pia wakikabiliwa na michuano ya kombe la Shirikisho inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).
Chanzo: Mtanzania