Na Muhsin Juma
AHlAN wasahlan mpenzi msomaji wangu wa Jamvi la Kulonga ni Ijumaa nyingine tunakutana Jamvini katika kujadili na kuchambua habari za wanamuziki na matukio mbalimbali yaliyojiri na yanayotarajiwa kutokea katika tasnia ya sanaa na burudani.
Katika Jamvi la Kulonga leo ningependa kujadili ukimya wa Kampuni ya Makukwe Entertainment iliyo chini ya nyota wa zamani wa Tukuyu Stars na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambaye kwa sasa ni diwani wa Kata ya Vijibweni, Kigamboni jijini Dar es Salaam Suleiman Mathew, ambayo iliamua kuanzisha programu ya kusaka vipaji vya wanamuziki vijana wa muziki wa dansi, kwa kuanzisha shindano lililopewa jina ‘Music Dance Competition’ ili kuwaendeleza na kuwa warithi mikoba ya wakongwe waliokwisha kufariki dunia na wanaotarajia kustaafu.
Kuanzishwa kwa shindano hilo ilikuwa ni neema kubwa kwa tasnia ya muziki wa dansi ambao nadiriki kusema unachechemea kutokana na wanamuziki wengi kufariki na kukosekana kwa warithi wa nafasi zao kwa sababu ya vijana wengi kujikita katika kuimba muziki wa kizazi kipya yaani ‘Bongo Fleva’.
Jamvi hili likiwa mdau mkubwa wa muziki wa dansi sambamba na wadau wengine lilivutiwa na mpango wa shindano lakini zaidi ni muitikio wa vijana wengi wenye vipaji kutoka mikoa mbalimbali waliokuwa wamejitokeza katika Ukumbi wa Msasani Club kufanya usaili wa kushiriki katika kinyang’anyiro hicho huku wakisailiwa na wakongwe wa muziki huo nchini wakiongozwa na Abdul Salvador ‘Father Kidevu’ mpiga kinanda wa zamani wa Bima Lee Orchestra.
Zaidi ya vijana 100 wenye vipaji waliojitokeza katika kinyang’anyiro hicho kabla ya kuchujwa na kubakia 50 waliwekwa kambini na kuanza mazoezi ya kujifua sauti na matumizi ya vyombo ambapo Father Kidevu aliendesha zoezi la kuwanoa vijana hao akishirikiana na jopo la wanamuziki wengine ambao pia walikuwa ni majaji nao ni Nyota Waziri, Tshimanga Kalala Asosa na Ally Choki.
Kimsingi vijana hao waliwekwa kambini chini ya Kampuni ya Makukwe kwa lengo kupikwa ili baadaYe waje kushiriki shindano hilo la kusaka vipaji ambavyo vingeendelezwa na ikiwamo kutafutiwa ajira katika bendi mbalimbali ili kuziba nafasi kustaafu ili kuhakikisha muziki wa dansi hautetereki kwa kukosa vijana wenye ujuzi wa kutunga na kuimba na kujua matumizi ya vyombo kama ilivyo tatizo kwa wale vijana wanaopiga Bongo Fleva.
Jamvi hili lilikuwa mdau wa kwanza kumpongeza Mathew kwa kuwa alikuwa amefikiria wazo ambalo hata wanamuziki na wadau wa muziki huo hawakuwa nalo akilini kwa miaka mingi katika kufanikisha safari ya kunusuru muziki huo ambao umeshaanza kwenda mrama kama si kupotea katika medani ya kitaifa na kimataifa lakini swali ambalo Jamvi linajiuliza shindano hilo na wale vijana waimbaji waliokuwa wameanza kuonyesha uwezo wao wako wapi.
Hapa ndipo hoja ya msingi ya Jamvi hili inapotaka kujikita kuhoji na kupata majibu kutoka kwa kampuni hiyo nini kimekwamisha mchakato huo kwa miaka miwili ambao ulikuwa unatajwa katika karne hii kuwa ungekuwa na manufaa makubwa maendeleo ya muziki wa dansi ambao umewekwa kapuni na vyombo mbalimbali vya habari jambo linalotajwa kuwa ni moja sababu zinazochangia kuangukia pua kwa muziki huo huku ule wa kizazi kipya ukipewa sapoti kubwa.
zilizoachwa na wakongwe ambao wameshatangulia mbele ya haki na wanaotarajia Jamvi hili linawauliza Makukwe nini kimekwamisha mchakato huo ambao ulikuwa na sura ya kitaifa na kusadia kukuza vipaji ambavyo vingeweza kuwa msaada mkubwa kwa taifa lakini hadi leo hatuambiwi nini kimekwamisha mchakato huo.
Lakini zaidi ni kwamba kama mchakato umekwama kwa sababu ya kukosa udhamini ni vema wadau wakaelezwa pengine wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuisadia Makukwe iliyochini ya Mathew kufanikisha mipango iliyonayo ya kuibua vipaji hivyo ambavyo ni tegemeo kwa taifa siku za usoni.
Kwa namna yoyote ni wakati wa kampuni hiyo kuwaeleza watanzania mchakato huo umekwama nini ili waweze kutambua nini kinaendelea kuliko ukimya ambao umetanda lakini pasipo kujua lini litakuwepo shindano hilo muhimu kwa maendeleo ya muziki wa dansi.
Jamvi hili linautazama kwa jicho la tatu muziki wa dansi kama mtoto yatima kutokana na kila kukicha kuzidi kuyumba na kukalia kuti kavu kutokana na wenye muziki wao kukosa namna ya kuukuza na kuuendeleza kwa kukosa mipango ya kusaka warithi wa wakongwe wa bendi zao ambao wengi wameshafariki dunia na wengine wapo hai lakini wakiwa katika hatua za mwisho kustaafu.
Wakati Jamvi hili likitoa changamoto kwa Makukwe ni vema na bendi zenyewe zilizosalia kuanza mchakato wa kusaka vipaji pasipo kutegemea mtu mwingine awaandalie mpango mkakati wa kuibua wanamuziki, watunzi na wapiga vyombo ambao wamekuwa ni ombwe kubwa la muziki wa dansi nchini.
Ukweli ni kwamba bendi za muziki huo na wadau wake kwa maana ya wamiliki wameshindwa kuandaa vijana wa kuchukua nafasi za wakongwe hao jambo ambalo jamvi hili linaona ni kujimaliza wenyewe hasa kwakuwa hazina programu ya kuwaandaa vijana ambao watakuwa warithi wa baadaye na kwa dharau hiyo bendi nyingi zimekufa kibudu kama si kupoteza mashabiki.
Jamvi hili likiwa ni mdau mkubwa wa muziki huo linaona ni wakati muafaka kwa bendi kongwe za muziki huo zikiongozwa na Msondo Ngoma Music na Mlimani Park Orchestra kuandaa programu za kuandaa vijana kama nilivyowahi kuelekeza siku za nyuma kwenye jamvi hili.
Pengine Jamvi hili lichukue fursa ya kuipongeza Kampuni ya Aset chini ya ‘Iron Lady’ Asha Baraka, kwa uamuzi wake wa kuanzisha programu ya kufundisha vijana muziki na matumizi ya vyombo kwa malengo ya kuwaendeleza vipaji vyao, jambo linalopaswa kuigwa na bendi nyingine.
Kwa leo nalikunja Jamvi hadi wiki ijayo.
Chanzo: Tanzania Daima