Herieth Makwetta
WIKI hii tumekuletea prodyuza Villy David ambaye si mwenyeji sana machoni mwa wengi, lakini kutokana na nyimbo zake kadhaa alizowahi kutayarisha, zinamtambulisha yeye ni nani.
Bila shaka utakumbuka Badman ya D Knob aliyomshirikisha Cannibal kutoka nchini Kenya, bila kusahau Money Power Respect wa Country Boy na Scola wa Endru G ni baadhi ya nyimbo zinazomweka sokoni prodyuza Villy.
Una taaluma yoyote katika kazi hii?
Mh…sikusomea kwa kwenda shule au chuo. Ni kipaji zaidi lakini nimepata mafunzo kidogo ya recording na mixing toka studio tofauti
tofauti(Kamakawa Records na Metro Studios).
Kuhusu elimu yako ya nyuma na ni lini ulianza kazi ya utayarishaji wa muziki na nani hasa alikufunza.
Nimesoma shule ya msingi Minazi Mirefu(Ukonga Banana), sekondari nimesoma Pugu huku kidato cha sita nimemaliza katika Shule ya Sekondari ya Benjamin Wiliam Mkapa High School.
Baada ya kumaliza shule nilikuwa na mapenzi sana ya kupiga kinanda(piano) ambayo nilipewa na baba. Vilevile nilikuwa na kompyuta nyumbani ndio nikaanza kujifunza kutengeneza ala na kujisomea “articles”
mbalimbali zinazohusu uzalishaji wa muziki na sauti pia.
Lakini vilevile nilipata msaada kutoka kwa “rafiki yangu mkubwa” Marco Chali(ambaye tumekua wote) na Arthur wa Agies Records. Bila kumsahau Enrico wa Sound Crafters ambaye pia alinipa ujuzi kidogo.
Ulianza kufanya kazi hii katika studio gani na wimbo upi ulikuwa wa kwanza kutengeneza na kufanya vizuri?
Kama mtayarishaji wa muziki nilianza studio iliyokua inaitwa Vinice Productions maeneo ya Mikocheni mwaka 2008 mwishoni. Wimbo wangu wa kwanza kabisa kwenda redio ulikua unaitwa “Choo Cha Kike” ambao alifanya
Ommy G na D Knob lakini nyimbo iliyofuata ambayo ilikua inaitwa “Badman” ambao alifanya D Knob na Cannibal ilifanya vizuri sana na ndio ilionitambulisha sana. Kisha nikatoa wimbo wa Endru G na Temba unaitwa Jinsi Alivyo. Bahati mbaya siku chache zilizofuata studio iliibiwa hiyo ilikua Machi 2009.
Mwaka huo mwishoni nikaingia mkataba na studio inaitwa 24/7 Records iliyoko Mikocheni ambako nilitoa nyimbo kama Money Power Respect ya Country Boy, Scola ya Endru G na Barnaba, Club Anthem na Bora Tumeachana ya D.Knob na Matonya.
Nilikaa studio hiyo mpaka mwaka 2011 mwishoni. 2012 mwanzoni nilikutana na Mb Dogg tukaanza kufanya naye projects zake katika studio zake zinazoitwa Makopa Inc ambazo zipo maeneo ya Makuburi Mabibo na mpaka hivi sasa ndiko ninakofanyia kazi zangu.
Mpaka sasa ni ngoma ngapi ulizozitengeneza na zimeweza kufanya vema
Badman ya D Knob na Cannibal, Jinsi Alivyo ya Endru Gee na Temba, Money Power Respect ya Country Boy Godzilla na Quick Rocka, Scola ya Endru Gee na Barnaba, Club Anthem ambayo ilikua collabo ya wasanii tofauti(Stopa Rhymes,Quick Rocka,D Knob na Godzilla),
Bora Tumeachana ya D Knob na Matonya, One Minute ya Godzilla inc, Digidigi ya Hans Brain na Chibwa, Supastaa ya Dullayo…na nyingine nyingi tu.
Ni wasanii wapi ambao unajivunia kuwa nao au kuwatoa kwa kazi ya mkono wako?
Najivunia sana wasanii wote niliofanya nao kazi kuanzia kina D Knob, Endru Gee, na hasa Hans Brain kwa sababu huyu nilianza naye tangu akiwa underground na ameanza kutambulika na nyimbo yake ya Digidigi
inafanya vizuri sasa kwenye tv mbalimbali na kiukweli hatukutoa audio yake lakini ile video tu peke yake imemtambulisha sana na najivunia sana hilo.
Prodyuza gani unamkubali ndani na nje ya nchi?
Kwa hapa ndani nawakubali sana maprodyuza walioanza kina Master J, P Funk, Enrico, Mika Mwamba na Roy kwa sababu wao wameonesha njia. Nje nasikiliza sana kazi za Dr Dre na Timbaland, Pollow Da Don pamoja na Alex Da Kid. Timbaland na Dre hao ni kama ‘my heroes’ kwenye muziki na ni maprodyuza walionivutia sana.
Unadhani kuna siku katika muziki mambo yatabadilika?
Ndio hata sasa kuna mabadiliko makubwa sana na yanatia moyo, tunaona muziki ukizidi kukua wasanii wetu wakivuka mipaka na kufanya shoo kubwa tofauti na mwanzoni ambapo muziki ulikua ukionekana kama uhuni tu.
Nini makosa ya wasanii yanayopelekea washindwe kufikia malengo yanayopaswa?
Tatizo liko kwenye kujifunza zaidi na kutokuwa na mipango au malengo. Wanajikuta wanalewa umaarufu kidogo na kusahau kwamba ile ni kazi inayowalipa na mwisho wa siku wanajikuta wakipoteza mwelekeo.
Unapata usumbufu gani kutoka kwa wasanii unapofanya nao kazi?
Kutokuwa ‘serious’ wakati wa kazi au hata msanii mwingine anakuja studio hajajitayarisha hivyo utajikuta kazi ya saa moja inachukua masaa matatu au zaidi.
Nini kinakwamisha muziki wa bongo ushindwe kusonga mbele
Muziki wetu umekuwa kama hauna mwenyewe na umekosa usimamizi na utaratibu mzuri.
Nini matatizo unayokumbana nayo ukiwa kama prodyuza ambayo yanahitajika kurekebishwa?
Tatizo langu kubwa ni muziki kwa hapa Tanzania bado haujatambulika kama biashara au kazi rasmi. Kiasi kwamba huwezi kupata labda vitu kama mikopo ya kibenki labda ungewekwa utaratibu mzuri ungesaidia sana kiwanda cha muziki kukua zaidi.
Nini matarajio yako ya baadaye?
Natarajia kuvuka mipaka na muziki wangu utambulike kimataifa, tayari nimeanza kujipanga na hilo. Nina nyimbo mpya kadhaa ambazo zitaanza kutoka mwaka huu na mwakani itakua na mabadiliko makubwa sana.
Vile vile tuna ‘audition project’ ambayo tunategemea itaanza karibuni pamoja na kampuni inaitwa Dmajic pia tutakua tukiandika nyimbo mbalimbali za wasanii.
Chanzo: Mwananchi