Na Dina Ismail
KUTOKANA na vifo vya mashabiki zaidi ya 74 vilivyotokea nchini Misri, Ubalozi wa Misri nchini Tanzania umesema mpaka sasa hauna uhakika kama wapinzani wa Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Zamalek, itakuja nchini Februari 17, mwaka huu kama ilivyopangwa awali au la.
Zamalek ilipaswa kuja nchini kwa ajili ya mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya ligi hiyo, mchezo unaotarajiwa kupigwa Februari 18, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo vurugu zilizotokea Jumatano wiki hii na kusababisha watu 74 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 1,000 kujeruhiwa katika ghasia zilizotokea mjini Port Said, Misri baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu kati ya Al-Masry na Al-Ahly imeleta machafuko makubwa katika historia ya soka ya Misri.
Vurugu hizo zimesambaa katika maeneo mbalimbali ya nchi ya Misiri ambapo maelefu ya watu wamejitosa kwenye Uwanja wa Tahriri mjini Cairo kutaka serikali ya mpito iwajibike.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana juzi katika ofisi za Ubalozi wa Misri nchini, hakuna taarifa zozote zinazoendelea kuhusiana na ujio wa Zamalek ambayo mashabiki wake wameungana na wapinzani wao wa Al Ahli kutaka serikali iwajibike.
“Kweli tulishaanza mipango ya ujio wa Zamalek hapa nchini lakini kwa hali hii tumesimamisha kila kitu mpaka Jumatatu ya wiki ijayo ‘kesho’ ndiyo tutajua nini kinachoendelea,” alisema.
Kabla ya kutokea kwa maafa hayo, kulikuwapo na taarifa za msafara wa watu 34 kutoka huko wakiwamo wachezaji na viongozi ambao ulitarajiwa kuwasili nchini alfajiri ya Februari 17 na kufikia katika Hoteli ya Golden Tulip kabla ya kucheza mechi hiyo siku inayofuata na kuondoka Februari 20.
Kutokana na machafuko hayo, Waziri Mkuu wa Misri, Kamal el-Ganzouri, amewafukuza kazi viongozi wote wa Shirikisho la Soka la Misri (EFA) sambamba na kuagiza Jeshi la Polisi kuwahoji juu ya vurugu hizo na FIFA bado haijasema chochote.
Mara zote Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) huiondolea uanachama wake nchi yoyote ambayo viongozi wa kiserikali huingilia mambo ya kisoka kama alivyofanya Waziri Mkuu wa Misri.
Source: Tanzania Daima