Tuesday , 25 October 2016
Latest News

Wanafunzi wawili CBE wafa ajalini

WANAFUNZI wawili wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) wamefariki dunia jijini Dar es Salaam juzi katika ajali ya gari iliyotokea katika viwanja vya Shabaha.

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema ilikuwa saa 12 jioni, barabara ya White Sands, Mbezi Beach, baada ya gari lenye namba za usajili T 958 AXK aina ya Carina kuacha njia na kugonga mti.

Kamanda Wambura aliwataja waliofariki dunia eneo la tukio kuwa ni Ibrahim Kaliki (21) mwanafunzi wa CBE Mwanza na Samwel (23) anayesoma CBE Dar es Salaam.

Aliwataja majeruhi wengine katika ajali hiyo kuwa ni Christina Ami (20) mfanyabiashara na Maxon Kimaro (21) mwanafunzi Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kamanda Wambura, gari hilo lilikuwa likiendeshwa na George Deo (21), ambaye ni mwanafunzi wa CBE Mwanza,  likiwa na abiria watano wakitokea Whitesand Hotel kuelekea Barabara ya Bagamoyo.

Alisema gari lilipofika eneo hilo lilimshinda dereva na kuacha njia kisha kugonga mti, kupinduka na kuingia mtaroni.

Kamanda huyo alisema majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo na maiti zote zimehifadhiwa hospitalini hapo huku Jeshi la Polisi likimshikilia dereva kwa mahojiano na uchunguzi wa ajali hiyo.

 Source: Tanzania Daima
VN:F [1.9.22_1171]
Rating: 0.0/10 (0 votes cast)
VN:F [1.9.22_1171]
Rating: 0 (from 0 votes)

About Abdul Diallo