Tuesday , 25 October 2016
Latest News

Aliowakataa Nyerere 1995 wataivusha CCM 2015?

KUNA tatizo kubwa la Watanzania wengi kuogopa ukweli wa historia na wapo wanafalsafa wanaoamini kuwa ukitaka kumficha kitu Mtanzania kiweke kwenye kitabu, wengi hawataki kusoma, wanapenda kusikia au kusimuliwa.

Wakati Watanzania wengi wakiamini kuwa busara za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere (hayati) ndizo zilizoweza kusaidia kwa kiasi kikubwa nchi hii iweze kujijengea heshima ndani na nje ya mipaka yake, wapo wanaopuuza.

Wapo wanaopuuza busara  na hekima za Nyerere lakini wapo wanaolia hadi leo wakikumbuka mwaka 1999 mwaka ambao Baba wa Taifa hili aliwaaga rasmi Watanzania aliowapenda baada ya kukutwa na mauti.

Wapo waliosema wazi kuwa wataendelea kuzienzi hekima za Nyerere, wataendelea kuchota busara zake na kamwe hawawezi kwenda kinyume na yale mazuri yaliyoweza kuasisiwa na Baba wa Taifa enzi za uhai wake, watavaa viatu vyake.

Kauli hizo na maneno ya kujifariji yaliwatoka wale waliokuwa wakimuogopa Nyerere, wale ambao hata siku moja hawakuweza kudhani kuwa ipo siku Nyerere atakufa, walijua kuwa si rahisi mtu mwenye hekima na busara akafa mapema.

Nyerere amekufa huku akijua kuwa Tanzania aliyoiacha aliiacha kwenye mikono salama ya kiongozi aliyempigania na aliweza kutamka wazi kuwa hawezi kuona nchi hii ikiangukia kwenye mikono ya viongozi wasiokuwa na sifa ya kutawala.

Zipo kauli alizoweza kuziongea Mwalimu Nyerere wakati wa mchakato wa kwanza na wa mwisho katika uhai wake wa kuhakikisha kuwa ameshiriki kumpata mgombea wa urais mwaka 1995 aliyemtaka.

Tatizo kubwa la Mwalimu Nyerere hakuwa mtu wa kuficha mambo, alikuwa mkweli, hali iliyosababisha baadhi ya viongozi wenzake wamuite kwa jina la utani la ‘Baba haambiliki’, kuwa Nyerere alikuwa mbishi, alikuwa na msimamo ambao akiusimamia haikuwa rahisi kumrudisha nyuma.

Ikumbukwe kuwa kazi kubwa ilikuwa kwenye mchakato mkali wa kumpata rais wa Awamu ya Nne, yalikuwapo majina kadhaa ya wanachama wa CCM waliojitokeza mwaka 1995 kuomba ridhaa ya chama hicho ili kuupata urais.

Kwa kuwa kazi ilikuwa ngumu na mchakato ulibeba sura ya wagombea kadhaa ambao Nyerere alikuwa hawataki, hakukubali kuona wale aliowaona kuwa sifa zao hazijitoshelezi wakipigiwa kura ya kuwa wagombea wa urais.

Nyerere alikuwa na chaguo lake, alifanya kila aliloweza ili kuhakikisha kuwa CCM inampata mgombea ambaye ni chaguo lake na alikubali kumnadi mgombea aliyemtaka, Benjamin Mkapa ili kuhakikisha kuwa anashinda kwenye uchaguzi wa mwaka 1995.

Jitihada za Nyerere zilikuwa kumnadi Mkapa ambaye alionekana kuwa mgeni sana kwenye macho ya Watanzania wengi pia alionekana hakuwa maarufu sana ndani ya CCM yenyewe, sifa nyingi alizijua Mwalimu wake Nyerere.

Kwa hali hii na kipindi kilichopita wapo wanaokumbuka kuwa kina nani ambao Nyerere hakutaka kuwaona wakitawala nchi hii wakati akiwa hai. Nyerere alitangulia mbele ya haki bila kuona utawala wa wale aliowakataa, alisema hawezi kuona nchi ikitawaliwa na hao.

Nyerere kafa na pengine hajui yanayoendelea Tanzania ya leo kuwa wale aliowakataa nao wamekufa au wapo hai na kama wapo hai wameweza kutimiza ndoto zao za kuwa watawala wa nchi hii baada ya kukataliwa na muasisi wa taifa hili.

Lakini wale wasiotaka kuijua historia hawapendi kukumbushwa haya ninayoyasema kuwa kukataliwa kwao na Nyerere kweli kunaweza kuwa sababu ya kuwafanya hata Watanzania wengine wawakatae?

Hivi Nyerere kwa uwezo wake mbona alikuwa kama binadamu mwingine wa kawaida, kweli ipo haja ya kuendelea kuamini kuwa ukikataliwa na Nyerere utakuwa pia umekataliwa na Mungu?

Kama Nyerere aliamini kuwa kiongozi mzuri ni yule atakayeweza kuamini kuwa Ikulu ni mahali patakatifu, Ikulu si mahali pa kwenda kufanya biashara, si mahali pa kwenda kusaini mikataba haramu ya madini na utoroshaji wa maliasili zetu.

Nyerere alionya kuwa kiongozi anayetaka kuingia ikulu lazima ajipime mara mbili kwa kuwa lazima ajiulize huko ikulu anakotaka kukimbilia kuna nini, mbona leo hii watu wanatumia mabilioni ya fedha kwa sababu ya kutaka kwenda ikulu.

Kilichompa mashaka Mwalimu Nyerere juu ya wale wenye dhamira ya kwenda kufanya biashara ikulu, alijua fika kuwa ikulu ikitumiwa vibaya inaweza kuwa mwanya wa kitovu cha maovu na uandaaji wa mipango mizito ya kuhujumu uchumi wan chi, Nyerere aliogopa.

Aliogopa kwa kuwa katika imani yake, utii na uadilifu aliokuwa nao alijua fika kuwa ili mtu aweze kuwa kiongozi wa nchi na anayestahili kuingia ikulu lazima nafsi yake iwe tayari kuwatumikia Watanzania na si mabepari wa mataifa makubwa duniani.

Kwa kuwa Nyerere amekufa, wapo wanaoamini kuwa hata mawazo yake yamekufa, misimamo yake imekufa na hana mamlaka tena kwa Watanzania na hana sauti itakayokuja kuwaambia au kuwakumbusha upya Watanzania kuwa hao niliowakataa mimi na ninyi endeleeni kuwakataa.

Wengi walimpuuza Nyerere baada ya mazishi yake na hawaoni mambo mazito na hali ya sintofahamu inayoendelea hapa nchini kuwa yote hayo si maono ya Nyerere isipokuwa Watanzania watakuwa wamekengeuka.

Waliokataliwa na Nyerere wanaamini kuwa mzimu wa Nyerere hauna nguvu tena ya kuwarudi na hauna nguvu za kuirudisha nchi kwenye mstari wake kwani nguvu za pesa zinaweza hata kuhamisha milima.

Nyerere amekufa akiwa maskini, hakufa akiwa bilionea, leo hii anashindwa kunyanyua kinywa chake kutoka kaburini, Butiama alikozikwa, hajui jinsi fedha zinavyotamka kumpata rais wa nchi hii wa mwaka 2015.

Haijulikani kama aliowakataa Nyerere mwaka 1995 kama wanaweza kuwa chaguo la kudumu la Watanzania mwaka 2015 kwa maana ya kudumisha na kuendeleza fikra mfu za Nyerere ambazo Watanzania wengi hawakumbuki tena kauli zake na wosia aliokuwa akiwapa Watanzania.

Hakika harakati zinazofanywa na wale aliokuwa akiwaogopa Nyerere kuwapa nchi kunatoa taswira halisi ya mmomonyoko wa nguvu za chama tawala huku vyama vya upinzani vikizidi kukwea na hayo yote yanaweza kuwa mawazo ya Nyerere ambaye hakutaka kuona dalili za utengano ndani ya taifa moja.

Kwa maana hiyo Watanzania bado wana nafasi ya kuendelea kutafakari, kujitathmini na kuendelea kuzienzi hekima za Mwalimu Nyerere, kweli alikuwa kiongozi wa taifa hili na muasisi, lakini naamini Nyerere alikuwa na vitu vya ziada ambavyo ni nadra kwa viongozi wengi wa Kiafrika kuwa navyo.

Wapo wanaopuuza usiku na mchana kauli za Nyerere na kuziona kuwa yalikuwa maoni yake na kwamba mtu yeyote mwenye akili anaweza kusema kuwa mimi namtaka huyo na huyu simtaki, kwa hali hiyo wapo wanaoyachukulia mawazo ya Nyerere kuwa hata aliowakataa wakati wake hawakuwa chaguo lake.

Chaguo kubwa la Nyerere lilikuwa ni Watanzania na katika uhai wake alifikiria kuifanya Afrika kuwa nchi moja kwa maana ya kuweza kuyaunganisha mataifa yote yawe ndugu, alitamani siku moja iwe hivyo, hakupenda vita, hakupenda ubaguzi wa rangi na hakupenda kuona nchi tajiri zikizikandamiza nchi maskini.

Nyerere hakupenda kuona viongozi wenye fedha nyingi ambazo hajui walikozipata wakipigania kuingia ikulu, aliamua kuwakataa mchana kweupe, ndiyo maana nauliza aliowakataa Nyerere mwaka 1995 wataivusha CCM mwaka 2015?

Imeandikwa na Christopher Nyenyembe

cnyenyembe@yahoo.com; 0754 301864, 0715 301864

Source: Tanzania Daima Jumatano

VN:F [1.9.22_1171]
Rating: 0.0/10 (0 votes cast)
VN:F [1.9.22_1171]
Rating: 0 (from 0 votes)

About Zanzibar Yetu