Thursday , 27 October 2016
Latest News

Walimu wapanga kukwamisha bajeti Wizara ya Elimu.

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimetangaza kutokubali kupitishwa kwa bajeti ya serikali ya mwaka 2013/14 hadi hapo madai yao yatakapokuwa yamelipwa.

Pia chama hicho kimeionya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuacha propaganda za kuwasingizia kuwa wanatumiwa na chama kimoja cha upinzani kudai malimbikizo yao.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiel Olouch alipokuwa akifungua semina ya uundwaji wa katiba mpya, umuhimu na wajibu wa walimu wenye ulemavu katika ushiriki ndani ya katiba hiyo.

Akizungumza katika semina iliyofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la The Foundation For Civil Society, Olouch alisema kuwa serikali imekuwa na tabia ya kutengeneza propaganda za kukihujumu chama chao ili wasifanikiwe kudai madeni na haki zao za msingi.

Alisema serikali imeshindwa kukaa nao meza moja kwa lengo la kulipa madeni ya walimu na badala yake imekaa na kutengeneza propaganda kwamba CWT kinatumiwa na chama kimoja cha upinzani.

“Nataka kuwauliza ndugu zangu walimu, ni kweli sisi tunadai madeni yetu kwa kutumiwa na chama cha siasa? Serikali walituandikia barua wakieleza kuwa sisi tunatumiwa na chama kimojawapo cha siasa, japo hawakukitaja lakini si inajulikana wazi kuwa kwa sasa chama ambacho kina nguvu ni CHADEMA?

“Sasa CHADEMA ndicho kimeelekeza sisi tusilipwe fedha zetu, naeleza kuwa kamwe CWT hatutakubali serikali ikae pale bungeni kupitisha bajeti yake ya mwaka wa fedha 2013/14 bila kutulipa fedha zetu, ikishindikana tutafanya mambo makubwa zaidi ya yale ya mwaka jana,” alisema Olouch.

Aliongeza kuwa serikali pamoja na CCM wana makusudi ya kuwagawanya walimu ili wasipate nguvu ya kudai haki zao za msingi na ndiyo maana haitaki kukaa meza moja na walimu ili kutatua matatizo yao.

“Mpaka sasa walimu wanadai sh bilioni 25. Wapo walimu zaidi ya 70 ambao wanatakiwa kupandishwa madaraja, lakini bado hawajapandishwa na kuna walimu 6,000 wamepanda madaraja, lakini hawajarekebishiwa mishahara yao.

“Hayo yote tukiohoji tunaonekana tunatumiwa na vyama vya siasa hususani wapinzani jambo ambalo ni propaganda za kutaka kuwadhoofisha walimu wasidai haki zao,” alisema.

Oluoch aliongeza kuwa hawawezi kuendelea kupokea mshahara wa sh 270,000 kwa mwezi na kusisitiza kuwa serikali isipokubali kulipa madeni yao na kuwapandisha madaraja walimu waonastahili pamoja na kurekebisha mishahara yao watafanya uamuzi mgumu.

Naye mwakilishi na mratibu wa semina hiyo, David Kisamo alisema itasaidia kuwawezesha walimu kutoa maoni yao ni jinsi gani waweze kupata haki zao katika katiba mpya.

Alisema ili mwalimu aweze kufanya kazi zake vizuri, ni lazima katiba imtambue na kumpa kipaumbele tofauti na ilivyo sasa kwani walimu wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu.

Alieleza kuwa ugumu wa maisha kwa mwalimu ambao unasababishwa na serikali unawafanya kutotambua haki zao na kujikuta wanagawanyika.

Imeandikwa na

 Danson Kaijage, Dodoma

 

Source: Tanzania Daima

VN:F [1.9.22_1171]
Rating: 0.0/10 (0 votes cast)
VN:F [1.9.22_1171]
Rating: 0 (from 0 votes)

About Zanzibar Yetu

Comments are closed.