Monday , 24 October 2016
Latest News

BAJETI YA WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO KWA MWAKA 2012 – 2013.

HOTUBA YA WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO, MHE. DKT. FENELLA E. MUKANGARA(MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA BAJETI  KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013

UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo kwenye Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, sasa naomba kutoa hoja ya kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Asasi zake katika mwaka wa fedha wa 2012/2013.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana tena kwenye Bunge lako tukufu tukiwa wenye afya na uzima. Namshukuru pia kwa kuijalia nchi yetu kubaki katika hali ya amani na utulivu. Aidha, sina budi kukushukuru wewe binafsi na waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano mzuri mnaonipa unaoniwezesha kutekeleza kikamilifu majukumu niliyokabidhiwa.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa dhati Rais  wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa heshima aliyonipa ya kuniteua kuwa Waziri anayesimamia Sekta za Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na pia kumteua Mheshimiwa  Amos Gabriel Makalla (Mb), Mbunge wa Jimbo la Mvomero kuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Aidha, namshukuru Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi (Mb), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ushirikiano na maelekezo yake ya kazi wakati akiwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Nashukuru pia familia yangu, hasa mume wangu mpendwa, Prof. Daudi Mukangara na watoto wangu Cleopatra, Natasha na Jackson, kwa ushirikiano na uvumilivu wao muda mwingi ninapokuwa nikitekeleza majukumu ya Kitaifa.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/12, Bunge lako Tukufu liliwapoteza Mheshimiwa Jeremia Sumari, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki (CCM), Mheshimiwa Regia Mtema, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA) pamoja na Mheshimiwa Mussa Khamis Silima aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini (CCM). Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi.
Mheshimiwa Spika, napenda kwa namna ya pekee niwapongeze Mawaziri na Naibu Mawaziri pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pongezi za pekee ziwaendee Wabunge wote wapya waliochaguliwa na wananchi na walioteuliwa na Mhe. Rais na ambao wamejiunga katika Bunge lako tukufu kutoka katika Chama cha Mapinduzi, CHADEMA na NCCR – Mageuzi.
Mheshimiwa Spika, kipekee nitumie fursa hii kumpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuteua wajumbe wa Tume ya Katiba wenye dhamana ya kuratibu maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya.Vilevile, nawapongeza Mawaziri waliotangulia kuwasilisha hoja zao, hususan Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), kwa hotuba yake fasaha yenye maelekezo ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013. Waziri Mkuu ameainisha malengo ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kutokana na Dira ya Taifa ya Maendeleo, Malengo ya Milenia na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II).
Aidha, nampongeza Mhe. Stephen Wassira (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kwa hotuba yake iliyoonyesha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2011 na Mpango wa Maendeleo wa mwaka wa fedha 2012/2013. Pia, nampongeza Mhe. Dkt. William Mgimwa (Mb), Waziri wa Fedha, kwa hotuba yake nzuri iliyoainisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kwa namna ya pekee niwashukuru Waheshimiwa Wabunge waliochangia hotuba za Mawaziri walionitangulia. Maoni waliyotoa yamesaidia kuboresha mipango ya Serikali katika sekta mbalimbali, zikiwemo Sekta ambazo ziko chini ya Wizara ninayoiongoza.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya awali, naomba sasa kutumia fursa hii kuipongeza na kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ambayo inaongozwa na Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mhe. Jenista Joakim Mhagama na Makamu Mwenyekiti wake Mbunge wa Jimbo la Kondoa Kusini, Mhe. Juma Nkamia, kwa kuiongoza vizuri Kamati hii. Aidha, naishukuru Kamati  ya Bunge lako Tukufu kwa kutoa ushauri na maelekezo wakati wa kujadili bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Mheshimiwa Spika, hotuba yangu imegawanyika katika maeneo makuu manne kama ifuatavyo: Eneo la kwanza ni majukumu ya Wizara, eneo la pili ni Mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012, eneo la tatu linahusu Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa fedha 2012/2013 na eneo la nne nihitimisho lenye kujumuisha shukranimakadirio ya bajeti kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 na maombi rasmi ya fedha kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa mwaka wa fedha 2012/2013. 
MAJUKUMU YA WIZARA
Mheshimiwa Spika, majukumu ya Wizara hii ni haya yafuatayo:-
Kuandaa na Kusimamia utekelezaji wa Sera za Sekta za Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali;
Kuratibu na kusimamia masuala ya maendeleo ya Vijana ili kuwawezesha kujiajiri na kujitegemea;
Kusimamia Vyombo vya Habari nchini;
Kuratibu tasnia ya utengenezaji wa sinema, maigizo, maonyesho na utoaji wa leseni;
Kusimamia utendaji wa Taasisi, Mashirika ya Umma, Wakala, Miradi na programu zilizo chini ya Wizara;
Kuendeleza, kuwezesha na kuratibu masuala ya kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI  KWA MWAKA WA FEDHA WA 2011/2012
Mapato na Matumizi
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2011/2012 Wizara ilipanga kukusanya Mapato ya jumla ya                                            Shilingi 766,907,385 kutoka vyanzo mbalimbali. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni, 2012 jumla ya Shilingi 682,374,217 zilikuwa zimekusanywa ambazo ni sawa na asilimia 89 ya lengo la makusanyo ya mwaka.  Mchanganuo wa makusanyo upo katika Kiambatisho Na. I. Kadhalika Wizara ilitengewa jumla ya Shilingi 14,671,877,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Fedha hizo zilijumuisha mishahara ya Wizara Shilingi  2,076,869,000 na ya Taasisi  Shilingi 5,991,270,000; Matumizi Mengineyo (OC) ya Wizara   Shilingi 3,806,163,200 na  ya Asasi zake Shilingi 2,797,574,800. Hadi mwezi  Juni, 2012 jumla yaShilingi 14,671,877,000 zilipokelewa na kutumika.

Miradi ya Maendeleo
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2011/2012 Wizara ilitengewa jumla ya Shilingi 3,880,851,000 fedha za ndani  kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Hadi kufikia mwezi Juni, 2012,Shilingi  3,600,000,000 zilikuwa zimetolewa na kutumika, sawa na asilimia 92.8. Miradi iliyotekelezwa ni Ujenzi wa Eneo Changamani la Michezo na  Mradi wa Upanuzi wa Usikivu wa TBC, eneo la kuimarisha mitambo ya Radio na Televisheni.
SEKTA YA HABARI
Mheshimiwa Spika, Waraka wa mapendekezo ya Kutungwa kwa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari umekamilishwa na kuwasilishwa kwenye ngazi ya juu kwa maamuzi ya Serikali na hatimaye Bunge lako tukufu katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2012/13. Aidha, kutungwa kwa sheria hii  kutaimarisha weledi na uwajibikaji wa vyombo vya habari hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Idara ya Habari imeendelea kukusanya taarifa mbalimbali za Serikali, kuandika habari na kuzitoa katika vyombo vya habari, kupiga picha za matukio mbalimbali ya kitaifa, kuzitoa katika magazeti na kuzihifadhi katika maktaba ya kumbukumbu ya picha kwa njia ya elektroniki.
Mheshimiwa Spika, kupitia Tovuti ya Wananchi, wananchi wanaendelea kupata haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni kwa uhuru katika masuala yanayowahusu. Tovuti imewawezesha wananchi kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na Serikali. Aidha, katika kipindi cha mwaka ulioanza Julai, 2011 hadi Juni, 2012, jumla ya hoja 38,247 zimepokelewa. Hoja 36,466 zimeshughulikiwa kwa kupelekwa katika Wizara na Taasisi husika ili kupatiwa majibu na ufumbuzi. Hoja nyingi zilihusu ucheleweshwaji wa malipo ya pensheni, mgao wa umeme, ukosefu wa maji, ajali kazini hasa kwenye migodi na mabadiliko ya Katiba. Hoja 1,781 hazikushughulikiwa kwa sababu hazikuihusu Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza uhuru wa upatikanaji wa habari na vyombo vya habari, Wizara imeendelea na usajili wa magazeti na majarida. Hadi mwezi Juni, 2012 jumla ya magazeti na majarida 763yalisajiliwa, hii ikiwa ni ongezeko la magazeti 52 kutoka mwaka jana. Magazeti yaliyosajiliwa kuchapishwa kila siku na yaliyo hai ni 14 na yale yanayochapishwa kila wiki ni 62. Aidha, magazeti matano (5) yaliyokiuka maadili ya uandishi wa habari yalipewa onyo.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Utangazaji imeendelea kukua kwa kasi na watu wengi wanazidi kuomba leseni za kuanzisha vituo vya utangazaji. Mpaka sasa kuna vituo 85 vya redio na vituo 26 vya televisheni. Mchanganuo upo kiambatisho Na. VI.  Kwa kipindi cha mwaka 2011/12 vituo vipya 12 vya redio na kituo kimoja (1) cha televisheni chenye kutoa huduma ya matangazo ya malipo (Subscription Sattelite TV) vimesajiliwa.
Mheshimiwa Spika, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limeendelea kuwa chombo mahiri cha utangazaji nchini likiwa na Idhaa tatu (3) za redio na mbili (2) za televisheni. Aidha, limeendelea kuongoza kati ya vyombo vya utangazaji vilivyopo nchini kwa kueneza usikivu wa matangazo yake kupitia vyombo vyake vya redio na televisheni katika eneo kubwa zaidi la nchi yetu. Jumla ya mitambo 22 ya redio za mfumo wa FM imejengwa Zanzibar na katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara, Arusha, Dodoma, Manyara, Kigoma, Shinyanga, Singida, Tanga, Tabora, Rukwa, Katavi, Morogoro, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Iringa na Kilimanjaro. Mitambo hiyo inarusha matangazo ya Idhaa mbili za TBCTaifa na TBCFM.
Aidha, kwa upande wa redio kuna mitambo 9 ya Masafa ya Kati inayorusha matangazo ya TBCTaifa katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Dodoma, Arusha, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Ruvuma. Na kwa upande wa Televisheni, mitambo ipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Dodoma, Tabora, Kigoma, Mwanza, Kagera, Mara, Lindi na Mbeya kwa mfumo wa analojia, na mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro kwa mfumo wa dijitali. Matangazo yake yanapatikana kwa satelaiti na kwenye mtandao wa DSTV ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, TBC ilishiriki kwa ufanisi mkubwa kufanikisha maadhimisho hayo. Aidha, vipindi vingi viliandaliwa na kurushwa.  Matangazo ya kilele cha sherehe yalirushwa moja kwa moja kwenye redio na televisheni. Vilevile vipindi vya elimu kwa umma, burudani na biashara vimeendelea kurushwa kama kawaida.
Mheshimiwa Spika, katika kupanua vyanzo vya mapato, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) imezindua Gazeti la Kiswahili la michezo la kila wiki, Spoti Leo, ambalo limepokelewa vyema na wasomaji. Aidha, Kampuni imekamilisha ukarabati na kuhamia Jengo lake la ofisi lililopo Barabara ya Mandela jijini Dar es Salaam. Kukamilika kwa jengo hili, kunatoa fursa ya uendelezaji wa jengo la Mtaa wa Samora kama kitega uchumi. TSN imeendelea kuimarisha magazeti yake ya Daily News, Sunday News na Habari Leo. Kampuni hii inajiendesha kwa faida, ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/12 imechangia gawio la Shilingi 16,000,000 kwenye mfuko mkuu wa Serikali.
Kamati ya Maudhui
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Maudhui ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Na. 10 ya mwaka 2003. Kamati hii inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sera ya Utangazaji ya mwaka 2003, Sheria ya Bunge Na. 3 ya mwaka 2010 pamoja na Kanuni za Utangazaji za mwaka 2005. Kamati hiyo inateuliwa na Waziri mwenye dhamana ya utangazaji. Kwa mujibu wa Kifungu cha 27 cha sheria hiyo, Kamati ina jukumu la kumshauri Waziri kuhusu masuala ya Sera ya Utangazaji nchini, kufuatilia na kudhibiti maudhui potofu ya utangazaji. Kamati pia inasimamia na kuhakikisha kuwa maadili na kanuni za utangazaji zinafuatwa. Aidha, Kamati inashughulikia malalamiko yatokanayo na maudhui ya utangazaji kutoka kwa watumiaji wa huduma za utangazaji nchini.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Maudhui imeendelea kupokea na kushughulikia malalamiko yatokanayo na vipindi vinavyorushwa ambavyo vinakiuka maadili ya utangazaji na utamaduni wa Mtanzania. Kamati imekuwa ikiyafanyia kazi malalamiko yote na kuyatolea maamuzi. Ilipobidi Kamati ilitoa makaripio kwa vituo vilivyokuwa vikienda kinyume cha sheria na kanuni za utangazaji za mwaka 2005 na maadili katika utangazaji. Katika kipindi hicho, Kamati ya Maudhui ilisikiliza mashauri manne (4) ya ukiukwaji wa Kanuni za Utangazaji. Katika kipindi cha mwezi Julai, 2011 hadi mwezi Juni, 2012 TCRA ilipokea jumla ya malalamiko kumi na nane (18)ambapo kati ya hayo kumi na tatu (13) yaliwasilishwa na wananchi na matano (5) yalitokana na ufuatiliaji wa wajumbe wa Kamati ya Maudhui. Vituo saba (7) vilipewa onyo na vituo viwili (2) vilipewa mwongozo. Aidha, Wizara yangu imeelekeza kuanzia sasa kila kituo cha utangazaji kiwe na Miongozo ya Sera za Uhariri (Editorial Policy Guidelines).  Miongozo hii itasaidia kuweka misingi ya vituo vya utangazaji ili kuviwezesha kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa. Vituo vitakavyokwenda kinyume na miongozo hii vitachukuliwa hatua na ikibidi kuvifungia.
Mheshimiwa Spika, TCRA kwa kushirikiana na Wizara yangu pamoja na wadau wa Sekta ya Utangazaji, imefanya marekebisho ya Kanuni za Utangazaji kufuatia kukua kwa Sekta ya Utangazaji na kubadilika kwa mfumo wa utangazaji hasa kuelekea kwenye mfumo mpya wa utangazaji wa dijitali. Aidha, naomba kuchukua fursa hii ya pekee kuwashukuru wadau wote wa Sekta ya Utangazaji kwa michango, mapendekezo na maoni yao katika kufanikisha zoezi lote la kuziandaa upya kanuni hizi. Kadhalika, shukrani zangu za dhati ziende kwa uongozi wa TCRA kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha zoezi hili.
Mheshimiwa Spika, kama mnavyofahamu mwaka 2011/2012, TCRA imefanya mikutano na wadau wa Sekta ya Utangazaji katika kutoa elimu kwa umma kuhusu mchakato wa kuhama kutoka teknolojia ya utangazaji ya analojia kwenda dijitali. Uhamaji huo unatakiwa uwe umekamilika ifikapo tarehe 17 Juni 2015, kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU).
Mheshimiwa Spika, nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki zimeazimia kusitisha matangazo ya analojia ifikapo tarehe 31 Desemba, 2012. Kiufundi, kusitisha katika kipindi hicho cha miaka mitatu kabla ya muda uliokubaliwa ulimwenguni, kutaziwezesha nchi wanachama kupata fursa ya kutathmini iwapo kutatokea matatizo ya kiufundi washirikiane kuyatatua mapema ili kuondoa usumbufu usio wa lazima. Pili, katika kipindi cha mpito makampuni yanayotoa huduma za utangazaji yatahitajika kuendelea kutoa huduma kwa mfumo wa analojia kwa maeneo ambayo mfumo mpya haujafika na pia kwa dijitali kwa mujibu wa Kanuni za TCRA. Hata hivyo, mchakato wa mabadiliko haya kutoka teknolojia ya analojia kwenda dijitali utagusa utangazaji kwa njia ya televisheni pekee na siyo utangazaji wa redio.
Mchango wa Vyombo vya Habari 
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuthamini mchango wa Vyombo vya Habari, ili kuimarisha Tasnia ya Habari nchini. Wizara yangu inaendelea kuhimiza Vyombo vya Habari kuhakikisha vinaajiri wahitimu bora wa taaluma ya uandishi wa habari na utangazaji. Umefika wakati kwa Vituo vya Televisheni kuwatumia wahitimu hao ili viweze kutoa matangazo bora kwa wasikilizaji na watazamaji. Kwa hili, nitaendelea kuhimiza ili kuhakikisha weledi wa uandishi wa habari unashamiri hapa nchini. Nahimiza pia matumizi ya lugha ya Kiswahili sanifu katika vituo vya televisheni na redio. Ni matumaini yangu vituo vyote vitawajibika katika matumizi bora ya Kiswahili sanifu, na vitajiwekea utaratibu wa kutathmini mwelekeo mzima wa lugha hii ya taifa ambayo ndiyo inayotumika kwa Watanzania wote.
Mheshimiwa Spika naomba kulipongeza Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa mchango wake katikakuboresha mitaala ya Mafunzo  kwa ajili ya Uandishi wa Habari. Mitaala hiyo ambayo  iliandaliwa na kupewa ithibati na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ni kwa ngazi ya 4 ya Cheti cha Awali cha uandishi wa habari (Basic Certificate in Journalism), ngazi ya 5  ya Cheti cha Uandishi wa Habari (Certificate in Journalism) na ngazi ya 6 ya Stashahada ya  Uandishi wa Habari (Diploma in Journalism). Kukamilishwa kwa mitaala hiyo na kupewa ithibati ya NACTE ni hatua muhimu katika kuimarisha mafunzo yanayotolewa kwa waandishi wa habari kwenye vyuo mbalimbali vya hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutambua juhudi zinazofanywa na Vyama na Taasisi mbalimbali za habari katika kuimarisha weledi, uwajibikaji na maadili ya uandishi wa habari kwa kuwatambua na kuwatuza waandishi wa habari ambao wamefanya vizuri zaidi. Chini ya uongozi wa Baraza la Habari Tanzania, vyama mbalimbali vya uandishi wa habari vimekubaliana kutoa tuzo za pamoja ambazo zinaheshimika kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na habari za afya, mazingira, biashara, michezo, sayansi na teknolojia, watoto na jinsia. Katika kufanikisha hili, mwezi Machi, 2012, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alikuwa Mgeni rasmi katika Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari za mwaka 2011.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuvipongeza kwa dhati Vyombo vya Habari  kwa kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Vyombo hivi vimehabarisha wananchi kuhusu maendeleo na mafanikio yaliyopatikana nchini mwetu katika kipindi hicho. Aidha, navipongeza vyombo hivyo kwa namna vilivyotoa taarifa kuhusu maafa makubwa yaliyotokana na mafuriko ya mwaka jana na kusababisha kupotea kwa maisha ya watu, mali zao pamoja na uharibifu wa miundombinu. Vyombo vya Habari vilikuwa bega kwa bega katika kutoa taarifa muhimu kwa wananchi, kuhamasisha uokoaji na utoaji wa misaada mbalimbali kwa wananchi walioathirika.
Mheshimiwa Spika, ni matumaini ya Wizara yangu kuwa juhudi hizi za pamoja kati ya Serikali na wadau wote wa habari zitaendelea katika kuimarisha Sekta ya Habari ili iendelee kutoa mchango mkubwa  zaidi katika kuharakisha maendeleo na ustawi wa nchi yetu.
SEKTA YA MAENDELEO YA VIJANA  
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kufanikisha utekelezaji wa Mwongozo wa Stadi za Maisha kwa vijana  walio nje ya shule. Kupitia Mwongozo huu ambao utasaidia  kukabiliana na changamoto za maisha, Wizara imewapa mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Vijana wote nchini ili waweze kuufahamu na hivyo kusimamia utekelezaji wake katika maeneo yao. Aidha, mtaala wa kufundishia stadi za maisha kwa waelimisha rika umeshaandaliwa.
Mheshimiwa Spika, Wizara imewezesha kuridhiwa kwa Mkataba wa Vijana wa Afrika wa mwaka 2006. Mkataba huu umeridhiwa na Bunge lako Tukufu mnamo tarehe 1 Februari, 2012.  Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imepeleka taarifa za kuridhiwa mkataba huo Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) ili nchi yetu iweze kuwekwa kwenye orodha ya nchi zilizokwisha ridhia mkataba huo.  Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanza kuchukua hatua za kuandaa muswada wa sheria ya utekelezaji wa mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2011 zilizinduliwa tarehe 14 Oktoba, 2011 katika Kijiji cha Butiama Mkoani Mara. Mgeni Rasmi wakati wa uzinduzi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal. Siku hii pia ni ya kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa na Muasisi wa Mwenge wa Uhuru, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Aidha, Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2011 zilikuwa maalum kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara chini ya kauli mbiu “Tumethubutu, Tumeweza na Tunazidi Kusonga Mbele”. Mbio hizo pia zilitumika kuwahamasisha wananchi na hasa vijana kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI, kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vya rushwa.  Sambamba na maadhimisho hayo Mwenge wa Uhuru pia ulipandishwa katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro usiku wa kuamkia Desemba 9, 2011 kukumbuka siku ya uhuru wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru zilifanyika Mkoani Dar es salaam tarehe 01 Desemba, 2011. Mgeni Rasmi katika sherehe hiyo alikuwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa kupitia Mbio za Mwenge, jumla ya miradi 273 yenye thamani ya Shilingi 232,357,556,185 ilizinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi.
Mheshimiwa Spika, Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2012 zilizinduliwa tarehe 11 Mei, 2012 katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mkoani Mbeya. Mgeni Rasmi katika sherehe hizo za uzinduzi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda. Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni, “Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo Yetu Shiriki Kuhesabiwa 26 Agosti, 2012”. Aidha, ujumbe huu unaambatana na kauli mbiu nyingine za uhamasishaji wananchi kuhusu mambo yafuatayo; Mabadiliko ya Katiba, Mapambano Dhidi ya UKIMWI, Rushwa na Matumizi ya Dawa za Kulevya. Sherehe za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2012 zitafanyika tarehe 14 Oktoba, 2012 katika Mkoa wa Shinyanga.
Mheshimiwa Spika,  Maadhimisho ya Wiki ya Vijana yalifanyika sambamba na Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyoadhimishwa mkoani Dar es Salaam. Vijana kutoka sehemu mbalimbali za Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania walishiriki. Aidha, katika banda la maonyesho la kila mkoa kulikuwa na uwakilishi wa shughuli za maendeleo ya vijana.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine imeadhimisha Siku ya Kujitolea Duniani mkoani Dar es Salaam. Sherehe za mwaka 2011 ziliadhimishwa sambamba na maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru.  Aidha, vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini wameshiriki katika makongamano ya kimataifa nchini Marekani, Australia, Guinea ya Ikweta, Kenya na Rwanda.
SEKTA YA MAENDELEO YA UTAMADUNI
Mheshimiwa SpikaWizara yangu imeratibu mchakato wa kuridhia Mikataba miwili ya UNESCO ambayo ni Mkataba unaohusu Kulindwa kwa Urithi wa Utamaduni Usioshikika wa mwaka 2003 na Mkataba unaohusu Kulindwa na Kukuzwa kwa Uanuwai wa Kujieleza Kiutamaduni wa mwaka 2005.  Aidha, hati  ya kuridhiwa Mikataba hii ilipelekwa UNESCO Makao Makuu na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO tarehe 8 Agosti, 2011. Katika kutekeleza Mikataba hiyo Wizara iliandaa mafunzo kwa wadau wa Sekta ya Utamaduni ili kujenga uelewa wa pamoja wa utekelezaji. Baadhi ya masuala yaliyomo katika Mikataba hiyo ni pamoja na utafiti, kuorodhesha amali na urithi wa utamaduni usioshikika, kuhifadhi, kusambaza na kukuza utamaduni kwa maendeleo ya jamii.
Mheshimiwa Spika,  katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/12 Wizara imeendelea kutoa elimu juu ya Utamaduni wa Mtanzania kwa jamii katika kutambua, kupokea na kuheshimu maadili yetu ya Kitanzania.  Elimu hii imekuwa ikitolewa kwa kuandaa na kurusha vipindi vya redio kuhusu ‘Maadili ya Mtanzania’  kupitia kituo cha TBCTaifa.   Katika kipindi hicho jumla ya vipindi 42 vilirushwa.
Mheshimiwa Spika Wizara yangu iliunda Kamati ya kukusanya maoni ya Wananchi kuhusu dhana ya kuwa na Vazi la Taifa. Maoni yalikusanywa kikanda na Wizara imepokea mapendekezo ya Vitambaa  kutoka katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Mapendekezo yaliyowasilishwa na wengi ni kuwa na kitambaa mahususi kitakachoshonwa Vazi la Taifa. Kutokana na hatua hiyo, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa utaratibu wa kupata Vazi hilo upo katika ngazi za ushauri Serikalini na matarajio yetu ni kukamilisha zoezi hili katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13.     
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha  2011/12  Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)  lilitekeleza kazi muhimu zifuatazo:-
Miswada 46 ya vitabu vya taaluma ilisomwa na kupewa ithibati ya lugha.
Baraza lilitoa huduma ya tafsiri ya miswada, brosha, hati mbalimbali kama vile vyeti vya shule, vyeti vya kuzaliwa, hati za ndoa na talaka.  Pia lilithibitisha tafsiri mbalimbali zilizofanywa na wafasiri wa nje.
Baraza liliratibu na kutoa huduma ya ukalimani wa Kiswahili kwenye mikutano ya Umoja wa Afrika iliyofanyika mwezi Julai, 2011 huko Guinea ya Ikweta na Januari, 2012 huko Ethiopia.  Aidha, Baraza lilitoa huduma ya tafsiri na ukalimani wa Kiswahili kwenye mikutano  ya Bunge la Afrika iliyofanyika mwezi Oktoba, 2011 huko Afrika Kusini.
Baraza lilichunguza makosa yanayofanywa na Vyombo  vya Habari na watumiaji wengine wa Kiswahili.  Jumla ya makosa 120  yalibainishwa na kuorodheshwa pamoja na usahihi wake. Makosa hayo yamekuwa yakisahihishwa katika vipindi vya redio na televisheni vinavyoshirikisha wataalamu wa BAKITA.
Mheshimiwa Spika,  katika kipindi cha mwaka  wa fedha 2011/12 Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lilitekeleza kazi zifuatazo:-
Kuendesha midahalo 47 ya Jukwaa la Sanaa ambapo jumla ya mada 47  ziliwasilishwa kwa wadau 4,055.  Midahalo hii inalenga kuwapa wadau uelewa mpana wa tasnia ya sanaa.
Kuendesha mafunzo kwa walimu 54  kutoka shule za Msingi 20 katika mkoa wa Morogoro. Mafunzo hayo yamewajengea uwezo walimu wa kuwapa stadi za uchoraji na utambaji  wa  sanaa watoto shuleni.
Kusimamia  uchaguzi  wa viongozi wa Mashirikisho manne (4) ya Sanaa za Maonesho, Ufundi, Muziki na Filamu kwa kupata viongozi wapya kwa mujibu wa katiba zao.
Kushiriki  katika Mkutano Mkuu wa Tano wa Shirikisho la Mabaraza ya Sanaa Ulimwenguni Australia na kujenga mahusiano na Mabaraza ya Sanaa ya mataifa mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/12 Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza imekagua jumla ya filamu 98 ambapo filamu za ndani 48 zilikaguliwa na kupewa madaraja. Kati ya hizo, 1 ilipewa daraja R ikimaanisha filamu hiyo hairuhusiwi kuoneshwa mahali pa hadhara. Filamu zilizokaguliwa  kutoka nje ya nchi ni 50,  kati  ya hizo,  3 zilipewa daraja R ambapo moja ni kutoka Liberia na mbili kutoka Norway. Aidha, Bodi imeweka alama maalum kwenye filamu zilizokaguliwa ikiwa ni moja ya njia ya kuhakikisha filamu zote zisizokaguliwa zinajulikana na wahusika kuchukuliwa hatua. Katika kipindi cha  mwezi Julai, 2011 hadi Juni, 2012 Bodi ilitoa vibali 21 vya kutengeneza filamu kwa Watanzania, na 84  kwa wageni.
Mheshimiwa Spika, Bodi ya Ukaguzi wa filamu na Michezo ya Kuigiza iliandaa na kufanya mafunzo elekezi kwa Maafisa Utamaduni wa Wilaya  nchini kwa lengo la kuboresha Bodi  za Filamu za Wilaya. Bodi ilisambaza Sheria na Kanuni za Filamu na Michezo  ya Kuigiza kwa Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi  wa Wilaya nchini.  Bodi imeendesha mijadala mitatu kwa wadau wakiwemo watengenezaji filamu na wasanii wa filamu.  Vilevile, imefanya mkutano kuhusu Mustakabali wa Tasnia ya Filamu katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru na mkakati kwa kipindi cha miaka 50  ijayo.  Mkutano huu umesaidia wadau walioshiriki kubuni mikakati mbalimbali ya kuboresha tasnia hii. Mikakati hiyo ni pamoja na kuhakikisha kuwa filamu na michezo ya kuigiza vinalenga zaidi katika kutangaza utaifa, uzalendo, maadili na utamaduni wa Tanzania. Nia ni kuondokana na filamu ambazo zimemezwa na tamaduni za nje. Vile vile, kuhakikisha kuwa tasnia ya filamu inakuwa rasmi ili ichangie pato la taifa na la msanii binafsi.
Mheshimiwa Spika, Bodi ya Filamu ilizindua Kanuni  za Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ambapo nakala 4,200  za Kanuni na nakala 4,200  za Sheria zilisambazwa. Aidha, utafiti uliofanywa na Bodi kwa kushirikiana na wadau wa filamu umebaini kuwepo kwa Makampuni 127 yanayojihusisha na uongozaji, utengenezaji, uzalishaji na usambazaji wa filamu kwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee. Makampuni  hayo yameajiri watu kati ya watatu (3)  na kuendelea na kwa pamoja yanatoa wastani wa ajira 508.

SEKTA YA MAENDELEO YA MICHEZO
Mheshimiwa Spika,  Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine wa Michezo, iliendesha kongamano maalum kuhusu Michezo kwa Amani na Maendeleo. Kongamano hilo lililenga  kuonyesha fursa za kutumia michezo katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya Kitaifa na Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, katika kushiriki mashindano ya kimataifa, Timu za Taifa ziliandaliwa na kuwezeshwa kushiriki katika Michezo ya Afrika.  Tanzania iliwakilishwa na zaidi ya wanamichezo 60 katika mashindano hayo yaliyofanyika nchini Msumbiji, mwezi Septemba, 2011.  Katika mashindano hayo, timu ya Taifa ya Mchezo wa Netiboli ilishika nafasi ya pili na kujinyakulia medali ya fedha. Aidha, timu hiyo ya Netiboli ilishiriki katika mashindano ya Netiboli ya Kimataifa yaliyofanyika Dar es Salaam ambayo yalishirikisha timu 8 kutoka mataifa mbalimbali.  Tanzania ilijinyakulia ushindi wa pili katika mashindano hayo.
Mheshimiwa Spika, Wizara iliendesha mafunzo kwa wanachuo 38 katika fani za Stashahada ya Elimu ya Ufundishaji wa Michezo na Stashahada ya Uongozi na Utawala wa Michezo katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya. Mafunzo ya muda mfupi yalitolewa kwa wadau wa michezo zaidi ya 300 katika Vituo vya Michezo Kanda ya Kaskazini, Arusha na Kanda ya Kusini, Songea. Aidha, katika kupima ubora wa walimu wa michezo, mfumo maalum wa kitaifa wa kutathmini sifa na kutoa madaraja ya Walimu wa Michezo mbalimbali ulianzishwa.  Mfumo huu umeanza kwa majaribio kwa michezo mitatu ya Riadha, Soka la Wanawake na Mpira wa Wavu kwa kushirikisha walimu 86 katika hatua ya awali. Utekelezaji wa mfumo huu upo chini ya mradi wa kuboresha maisha ya watoto milioni mbili walioko shuleni kupitia michezo (International Inspiration) ifikapo mwaka 2014. Katika hatua ya awali, Mpango unaendeshwa kwa kujumuisha shule 15 zilizoko Zanzibar na mikoa ya Arusha, Mwanza, Dar es Salaam na Ruvuma.
Mheshimiwa Spika, ushauri wa kitaalamu ulitolewa kuhusu miundombinu na vifaa bora vya michezo katika Mikoa  ya Mara, Dar es Salaam na Dodoma.  Ushauri huu ulitolewa kwa wadau mbalimbali wa michezo wakiwemo wamiliki na viongozi wa viwanja vya michezo zaidi ya 50. Sambamba na ushauri huu huduma ya kinga na Tiba kwa Timu za Taifa zilitolewa kwa Timu zilizoshiriki mashindano ya Nchi za Afrika huko Msumbiji, Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) na SHIMIWI iliyofanyika huko Tanga.
Mheshimiwa spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/12 Wizara imeboresha Uwanja wa Uhuru kwa kuufanyia ukarabati mkubwa na kuujenga katika umbo la “U”. Ukarabati huu utakapokamilika Uwanja utakuwa na uwezo wa kukaa watazamaji elfu ishirini (20,000).
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/2012 Baraza la Michezo la Taifa (BMT)  lilitekeleza kazi zifuatazo:-
Kujenga uwezo wa wafanyakazi wa Baraza la Michezo la Taifa na Vyama vya Michezo vya Taifa kwa kuwaandalia mafunzo kulingana na mahitaji yaliyopo. Watumishi 12 wa Baraza walishiriki mafunzo ya sheria ya ununuzi yaliyoendeshwa na PPRA.
Kushirikiana na Halmashauri za Manispaa, Miji na Wilaya kuhamasisha na kuendesha matamasha ya michezo kwa jamii. Matamasha haya yalilenga kujenga mahusiano na kuboresha afya ya jamii. Halmashauri zilizoshiriki ni Musoma, Magu, Mpwapwa na Ngara.
Kuanzisha na kuendesha mafunzo ya ufundishaji michezo kwa viongozi vijana kwa ushirikiano na Vyama vya Michezo vya Taifa na Baraza la Michezo la Uingereza (UK Sport International). Vijana walioshiriki mafunzo hayo walitoka Dar es Salaam (800), Arusha (750), Mwanza (350) na Ruvuma (450).
Kuendesha mafunzo ya muda mfupi ya ufundishaji kwa Walimu wa Michezo mbalimbali wapatao 500 katika Wilaya 10 za Tanzania Bara.
Kuandaa, kusimamia na kuendesha mafunzo ya Uongozi kwa Vijana kupitia michezo kwa washiriki wapatao 1,200 na pia kuwashirikisha katika mabonanza wanafunzi wapatao 2,000 wa shule za Msingi na Sekondari.
Kuanzisha mpango maalum wa mafunzo ya Uongozi wa Michezo kwa Wanawake.
UTAWALA NA RASILIMALI WATU
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Serikali imeidhinisha miundo mipya ya  kada za watumishi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Miundo hii imeainisha vizuri wajibu na sifa za Maafisa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika ngazi ya Mikoa, Wilaya na Halmashauri.  Kupitia miundo hii, Wizara sasa itaweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi kwani itakuwa na kiungo kizuri kati yake na ngazi za chini walipo wananchi. Nitumie fursa hii kuwaomba Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha kuwa wanawawezesha maafisa hao ili waweze kutumika ipasavyo katika kuleta matokeo tarajiwa.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha Utawala Bora na ushirikishwaji wa Wafanyakazi Sehemu za kazi, Wizara imekuwa ikifanya vikao vya Baraza la Wafanyakazi ili kutatua kero mbalimbali zinazowakabili watumishi wa Wizara. Aidha, Wizara imehakikisha kwamba Watumishi wapya waliojiunga na Utumishi wa Umma kwa mara ya kwanza wanapewa mafunzo elekezi ambayo lengo lake ni kuwapa mwelekeo wa utendaji katika Serikali ikiwemo kuwafahamisha matarajio ya mwajiri, taratibu za utumishi na maadili katika Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa SpikaWizara imeendelea na zoezi la kuwapandisha vyeo watumishi wanaostahili kulingana na miundo ya utumishi ya kada zao na kwa kuzingatia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1999 na 2008. Katika kipindi cha mwaka wa  fedha 2011/2012 watumishi 46 walipandishwa vyeo.  Aidha, Wizara imewezesha kutoa mafunzo kwa Watumishi 17, kati ya hao 2 wamemaliza mafunzo na 15 wanaendelea.
C: MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
IDARA YA HABARI
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013, Wizara itatekeleza yafuatayo:-
Kuratibu shughuli za Vitengo vya Habari vilivyomo katika Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala za Serikali na kutoa mafunzo ya utoaji habari za Serikali kwa Maofisa Habari wa Vitengo hivyo.
Kuendelea na mchakato wa kuanzisha mtandao wa kulinda na kuuza picha za viongozi na matukio mbalimbali ya kitaifa popote duniani kupitia mradi wa “e-commerce”. Mtandao huo utawawezesha wadau kupata picha hizi popote kutoka katika maktaba ya picha.
Kuchapisha machapisho mbalimbali ya Serikali likiwemo gazeti la Nchi Yetu.
Kupokea maoni ya wananchi kupitia Tovuti ya Wananchi na kufuatilia majibu ya hoja hizo.
Kukusanya na kuandika habari za matukio mbalimbali ya Kiserikali.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2012/2013, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linatarajia kuimarisha vituo vya televisheni ili kuongeza usikivu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2012/2013, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inalenga kutafuta fedha za mradi wa upanuzi wa kiwanda cha uchapaji na kukamilisha mkakati wa ubia wa kuendeleza viwanja vyake vilivyopo Dodoma na Dar es Salaam. Aidha, kampuni itaendelea na juhudi za kuinua ubora wa magazeti yake na kuimarisha usambazaji, hasa mikoani.
SEKTA YA MAENDELEO YA VIJANA  
Mheshimiwa spika, katika  kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 Wizara imepanga  kutekeleza malengo yafuatayo:-
Kumpata mshauri mwelekezi ili kufanya upembuzi wa mradi wa kuanzisha Benki ya Vijana. Mchakato huu utahusisha ukusanyaji wa maoni toka kwa wadau mbalimbali.  Tayari mawasiliano ya awali yamefanyika kati ya Wizara yangu na uongozi wa Benki Kuu ya Tanzania na Benki ya Wanawake, kwa lengo la kupata maoni ya kiufundi, uzoefu na mstakabali wa uanzishaji wa Benki hiyo. Lengo la kuanzisha Benki hii ni kuwa na chombo maalum cha fedha kitakachotoa mikopo nafuu na inayokidhi mahitaji halisi na uwezo wa Vijana.
Kuendelea na maandalizi ya awali yanayohusiana na mapendekezo ya kutungwa kwa sheria ya uundwaji wa Baraza la Vijana Tanzania. Rasimu ya Waraka wa Baraza la Mawaziri inayohusu suala hili tayari imeandaliwa na ipo katika ngazi za ushauri na maamuzi serikalini.
Kuboresha utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa kuzijengea uwezo SACCOS 242 ambazo tayari ni wateja wa mfuko huu.  Inatarajiwa pia kwamba mara Benki ya Vijana itakapoanzishwa, SACCOS zilizopo na nyingine zitakazoanzishwa ndizo zitakazokuwa wateja wakubwa wa Benki hiyo.
Kuwapatia mafunzo maalum ya muda mfupi ya kujiajiri, ujasiri na ujasiriamali wahitimu wa shule na vyuo mbalimbali.  Moja ya mikakati ya kutekeleza lengo hili ni kwa kutumia vituo vyetu vya vijana vilivyoko Ilonga – Kilosa, Sasanda – Mbozi na Marangu – Moshi.
SEKTA YA MAENDELEO YA UTAMADUNI
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013, Wizara kupitia Sekta hii itatekeleza yafuatayo:-
Kukamilisha utaratibu wa urasimishaji tasnia ya filamu na muziki ili wasanii wanufaike na kazi zao pamoja na kuchangia Pato la Taifa. Maelezo  ya kina kuhusu utaratibu huu yalitolewa ndani ya Bunge lako tukufu na Waziri wa Fedha wakati akiwasilisha Hotuba ya bajeti ya Serikali  kwa mwaka wa fedha 2012/13.
Kuendelea kukusanya taarifa muhimu zinazohusu Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kwa kushirikiana na Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali.
Kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya vitambaa vya kushonwa Vazi la Taifa yaliyokusanywa Kikanda kwa kuhusisha mikoa yote na makundi maalumu, wakiwemo vijana na wanawake.
Kufanya utafiti wa lugha za jamii 12 za Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Rukwa na Kagera kwa lengo la kukuza na kuhifadhi lugha za jamii zinazotafitiwa.
Kusimamia na kuendesha Mkutano Mkuu wa Sekta ya Utamaduni unaofanyika kila mwaka kwa kuwashirikisha wadau na watendaji wa sekta hii. Lengo la mkutano huo ni kupokea, kujadili na kupitisha maazimio na mustakabali wa Utamaduni nchini.
Kuandaa na kurusha vipindi 52 vya redio kuhusu Maadili ya Mtanzania. Vipindi hivyo vina lengo la kuelimisha jamii kutambua nini ni maadili na nini sio maadili ya Mtanzania, ili kuelekeza vijana na Watanzania wote kwa ujumla kuthamini maadili ya taifa letu.
Kuratibu na kusimamia maadhimisho ya Siku ya Utamaduni Duniani pamoja na vikundi vya ngoma za asili kushiriki katika maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limepanga kutekeleza kazi zifuatazo:-
Kuandaa na kurusha vipindi 52 vya “Lugha ya Taifa”, vipindi 52 vya “Kumepambazuka” katika redio na vipindi 52 vya “Ulimwengu wa Kiswahili” katika televisheni ili kupunguza matumizi ya Kiswahili ambayo siyo sanifu.
Kuendelea kusoma miswada ya vitabu vya taaluma na kuipatia ithibati ya lugha.
Kuratibu na kutoa huduma za tafsiri na ukalimani katika mikutano ya kitaifa na kimataifa, shughuli za mashirika, makampuni na watu binafsi.
Kuendelea kuchunguza makosa  ya Kiswahili yanayofanywa na Vyombo vya Habari na watumiaji wengine na kusambaza masahihisho yake.
Kuhamasisha matumizi sahihi ya Kiswahili Sanifu katika mabango, matangazo na lebo.
Kuchunguza maneno ya lugha za makabila na lahaja za Kiswahili yanayoweza kusanifiwa katika mikoa ya Kanda ya Mashariki, Magharibi, Kusini na Kati.
Kukarabati na kuboresha majengo  yaliyonunuliwa kutoka Shirika la Bima la Taifa ili yaweze kukidhi mahitaji ya kiofisi kwa ajili ya matumizi ya BAKITA.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepanga kutekeleza kazi zifuatazo:-
Kuratibu midahalo 52 kupitia Jukwaa la Sanaa kwa Wasanii, Waandishi wa Habari 4,500 ili kuwapa ufahamu, elimu na ujuzi katika masuala ya sanaa.
Kuhuisha kanzidata ya wasanii, vyama vya sanaa, mashirikisho na wadau.  Lengo kwa mwaka huu ni kupata taarifa mbalimbali za wasanii 2,000, vyama vya sanaa 50, mashirikisho manne (4) na wadau 100 wanaojishughulisha na kazi za sanaa.
Kuendesha Mafunzo kwa ajili ya utengenezaji wa batiki na uchapaji kwa Wakufunzi wa wasanii 20  kutoka mkoa wa Dar es Salaam na Singida.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2012/2013 Bodi ya Ukaguzi wa Filamu imepanga kutekeleza kazi zifuatazo:-
Kupitia miswada 105  ya filamu na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu maboresho ya miswada hiyo.
Kukagua filamu 105  na kutoa ushauri wa kitaalamu wa maboresho na kuziwekea madaraja na alama maalum filamu zote zitakazokaguliwa.
Kushirikiana na Kamati  ya Taifa ya utoaji vibali vya filamu, kutoa vibali 25 vya kutengeneza filamu kwa raia wa Tanzania na vibali 100 kwa waombaji kutoka nje ya Tanzania.
Kutoa mafunzo ya kuongeza weledi kwa kushirikiana na wadau wa  tasnia ya filamu.
Kushirikiana na taasisi nyingine, kufanya  msako maalum kukamata filamu ambazo hazijakaguliwa na kuwachukulia hatua za kisheria  wahusika.
Kuimarisha Bodi na Sekretarieti yake kwa kuwapa mafunzo na kuweka vifaa vya kisasa vya ukaguzi vinavyoendana na teknolojia ya kisasa.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 Taasisi  ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imepanga kutekeleza kazi zifuatazo:-
Kuendesha mafunzo ya Stashahada kwa washiriki 150 na mafunzo ya muda mfupi kwa wasanii 200 walio kazini.
Kuendesha mafunzo ya cheti cha “National Technical Award” (NTA) katika fani ya uzalishaji na usanifu wa muziki.
Kukamilisha mitaala ya shahada ya kwanza ya sanaa za maonyesho na sanaa za ufundi na kuwasilisha NACTE kwa madhumuni ya kupewa ithibati.
Kusimamia na kuendesha Tamasha la 31 la sanaa na Utamaduni wa Mtanzania.
SEKTA YA MAENDELEO YA MICHEZO
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 Wizara itatekeleza kazi zifuatazo:-
Kuendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi ya fani mbalimbali za Michezo kwa walimu na viongozi wa michezo 400 katika Vituo vya Michezo Kanda ya Kaskazini (Arusha) na Kanda ya Kusini (Songea).
Kuendelea kusimamia utekelezaji wa tafiti kuhusu fani mbalimbali za Maendeleo ya Michezo.
Kusimamia uanzishwaji na utekelezaji wa mikataba ya ushirikiano kati ya Tanzania na nchi marafiki kuhusu ushirikiano katika Sekta ya Michezo.
Kuendesha mafunzo ya Stashahada ya Elimu ya Ufundishaji Michezo na Stashahada ya Uongozi na Utawala wa Michezo kwa wanachuo 40 wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
Kuwezesha Timu za Taifa kushiriki katika michezo ya Olimpiki na Paralimpiki Uingereza.
Kuendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya uendelezaji wa awamu ya pili ya ujenzi wa eneo Changamani la Michezo la Taifa lililoko Jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 Baraza la Michezo la Taifa (BMT) litatekeleza kazi zifuatazo:-
Kuendesha mafunzo ya muda mfupi kwa Walimu wa Michezo wapatao 3,000 nchini kwa kushirikiana na Halmashauri za miji na Manispaa.
Kutoa mafunzo ya elimu ya michezo na kupanga wataalamu wa michezo katika viwango stahiki (madaraja) kwa kushirikiana na Vyama vya Michezo vya Taifa.
Kuendelea kutoa mafunzo ya Utawala Bora kwa Viongozi wa Vyama vya Michezo vya Taifa kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija katika Sekta ya Michezo. 
Kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Baraza la Michezo la Taifa na Vyama vya Michezo vya Taifa kwa kuwaandalia mafunzo kulingana na mahitaji yaliyopo.
Kuendelea kusimamia mafunzo ya uongozi kwa Vijana kupitia michezo kwa walimu na vijana wa Shule za Msingi na Sekondari kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa.
Kuimarisha ushiriki wa wanawake katika michezo na uongozi wa michezo kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Uingereza (UK Sport International) kwa kuandaa mfumo wa utambuzi na uendelezaji wa vipaji katika michezo mbalimbali kupitia Mradi wa kuboresha maisha ya watoto (International Inspiration).
UTAWALA NA RASILIMALI WATU
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13, Wizara imepanga kuwaendeleza watumishi katika mafunzo. Wizara itaendelea kuwasomesha watumishi 21, kati ya hao  kumi na tano (15) ni wa mwaka wa fedha 2011/12, wawili (2) wapya, na wengine wanne (4) wanaotarajiwa kustaafu. Wizara itatoa mafunzo elekezi kwa watumishi ishirini (20), wanaotarajiwa kuajiriwa.
D: HITIMISHO
Mheshimiwa SpikaWizara yangu itaendeleza mafanikio yaliyopatikana katika   Sekta inazozisimamia ili ziweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya nchi yetu. Hii ni pamoja na kuongeza ajira, kipato, kulinda mazingira, kuleta amani na furaha katika jamii. Pamoja na kutumia fursa hizo bado kuna changamoto ambazo zinahitaji zipatiwe ufumbuzi ili kuzitumia ipasavyo katika kuleta maendeleo ya nchi. Matarajio yangu ni kwamba changamoto zilizopo zitaendelea kupatiwa ufumbuzi hatua kwa hatua hasa kwa kushirikiana na Sekta Binafsi na wadau wengine wa maendeleo.
SHUKRANI
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali na kwa niaba yangu binafsi naomba kuwashukuru kwa dhati wale wote walioshirikiana nasi katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012 katika kutimiza malengo yetu. Mafanikio ya utekelezaji wa majukumu na malengo ya Wizara yamewezekana kutokana na ushirikiano uliopo miongoni mwa viongozi na wafanyakazi wa Wizara na wadau wengine walio nje ya Wizara. Shukrani zangu za pekee ziende kwa  Mheshimiwa Amos Gabriel Makalla, (Mb), Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye amekuwa msaada mkubwa kwangu, Bw. Sethi Kamuhanda, Katibu Mkuu na Bibi Sihaba  Nkinga,Naibu Katibu Mkuu.
Aidha, nawashukuru Wakurugenzi, Wataalamu, na Watumishi wote wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Asasi zilizo chini ya Wizara kwa juhudi walizofanya kuhakikisha kwamba wanatimiza ipasavyo majukumu tuliyokabidhiwa na Taifa.
Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa nitumie fursa hii tena kuwashukuru washirika wetu wa maendeleo ambao wametuunga mkono wakati wote wa kutekeleza majukumu ya Wizara yangu.  Shukrani hizi ziwaendee wahisani waliotusaidia nikitarajia kuwa wataendelea na moyo huo.   Siyo rahisi kuwataja wote lakini nitaje wachache ambao ni Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Finland, Uingereza, Denmark, Japan, Sweden, Norway, Iran, Cuba, Korea ya Kusini, Marekani na Ujerumani pamoja na Mashirika ya kimataifa ya UNESCO, CYP, UNV, ILO, UNICEF, UNFPA, IYF na UNDP.
Mheshimiwa Spika, napenda kuvishukuru vyombo vyote vya habari nchini ambavyo vimefanya kazi nzuri ya kuitangaza nchi yetu. Ninaamini kuwa vyombo hivyo vitaendelea na kazi ya kuhabarisha, kuburudisha na kuelimisha umma kwa kuzingatia maadili. Aidha, ninamshukuru sana Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha hotuba hii kwa wakati, bila kuvisahau vituo vya Televisheni na Radio ambavyo kwa namna ya pekee vinarusha hotuba hii hewani.
MAKADIRIO YA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
Mapato
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 Wizara imepanga kukusanya jumla yashilingi 714,209,000 kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali vya mapato. Mchanganuo wa makusanyo kifungu kwa kifungu upo katika Kiambatisho Na. I.
Matumizi ya Kawaida 
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 Wizara imetengewa bajeti ya Shilingi 16,210,999,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida (Matumizi Mengineyo na Mishahara), fedha hizo zinajumuisha:-
Mishahara ya Wizara                   – Shilingi 2,410,357,920
Mishahara ya Asasi                    – Shilingi  7,761,301,000
Matumizi Mengineyo ya Wizara      – Shilingi 4,635,340,080
Matumizi Mengineyo ya Asasi        – Shilingi 1,404,000,000 
Mchanganuo wa makadirio ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara upo katika Kiambatisho  Na. II. Aidha, Matumizi ya Kawaida kwa Wizara peke yake yapo Kiambatisho Na. III na kwa Asasi yapo Kiambatisho Na. IV. 
Miradi ya Maendeleo
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 Wizara imetengewa jumla ya shilingi 3,096,600,000 kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo, Fedha za ndani ni  shilingi 2,740,000,000 na fedha za nje ni shilingi 356,600,000. Mchanganuo kamili upo katika Kiambatisho  Na.  V.
MAOMBI YA FEDHA KWA AJILI YA KUTEKELEZA MPANGO WA MWAKA 2012/2013
Mheshimiwa Spika, ili Wizara yangu iweze kutekeleza majukumu na malengo yake ya mwaka wa fedha 2012/2013, naomba sasa Bunge  lako  Tukufu  liidhinishe  bajeti  ya jumla ya shilingi 19,307,599,000 ambapo kati ya  hizo,  fedha za Matumizi ya Kawaida ni shilingi 16,210,999,000 na fedha za Miradi ya Maendeleo nishilingi 3,096,600,000.  Mchanganuo wa fedha hizi upo katika viambatisho nilivyovitaja hapo awali ambavyo ni sehemu ya Hotuba hii.
Mheshimiwa Spika, napenda nitoe tena shukrani zangu za dhati kwako binafsi na kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza. Hotuba hii inapatikana pia katika tovuti ya Wizara kwa anuani ya: www.hum.go.tz.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
VN:F [1.9.22_1171]
Rating: 0.0/10 (0 votes cast)
VN:F [1.9.22_1171]
Rating: 0 (from 0 votes)

About Dullonet Habari

Comments are closed.