Dullonet Tanzania | Kaseja aingia katika orodha ya makipa wafungaji duniani
Home                   Burudani               Chatroom            Contact Us             About Us                       Maintenance
Copyright @ 2007 Dullonet.com. All Right Reserved
Entertainment News
Website Designing
We're specialized in developing website's that work. .. More
PC Networking
The Networking  specialises in IT and Network Support ... More
PC Maintenance
PC Repair and Computer maintenance, for the home / business user... More
Mwimbaji mahiri wa taarabu nchini, Nasma Khamis 'Kidogo' amefariki dunia. Akizungumza Dar es Salaam jana, baba mdogo wa marehemu, Hamis Kaniki alisema Nasma alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi kutokana na homa ya malaria.

"Mara kwa mara Nasma alikuwa anasumbuliwa na matatizo ya moyo, ndio ugonjwa wake mkubwa, lakini miezi ya karibuni alipata nafuu akawa anafanya shughuli zake. "Lakini kuanzia Ijumaa alishikwa na homa ya malaria, ambayo iliibua tena matatizo ya moyo hadi mauti yalipomfika, " alisema Kaniki.

Alisema hadi mauti yanamkuta Nasma alikuwa akijishughulisha na masuala ya biashara pamoja na mifugo, ingawa pia usanii alikuwa akiendelea lakini akiwa anajitegemea. Alisema Nasma alizaliwa miaka 57 iliyopita Kilwa Kivinje na alibahatika kupata watoto wanane, ambapo sita wapo hai wakati wawili ni marehemu na kuwa maziko yatafanyika leo makaburi ya Kisutu Dar es Salaam.

Akizungumza kwa simu kutoka Biharamulo jana, mpapasa kinanda wa kundi la TOT Plus, Juma Abdallah 'JJ Mzee wa Mbezi', alisema amepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kifo cha Nasma maana yeye ndiye aliyempokea kwenye kundi la Tanzania One Theatre (TOT sasa TOT Plus) mwaka 1993 wakati msanii huyo alipokuwa akitokea Zanzibar.

"Kama kuna mtu anamfahamu vizuri Nasma, basi mimi ni mmojawao, maana ndiye nilimpokea kutoka Zanzibar alikokuwa akifanya shughuli za muziki, nikamkaribisha TOT na nilifanya naye kazi kwa karibu zaidi," alisema JJ.

Akiwa TOT, Nasma aliimba nyimbo za Kamba ya Mgomba, Koroboi, Ikwinini na Kidudu Mtu, kisha akajiunga na Kundi la Muungano Cultural Troupe, ambako alishiriki kuimba nyimbo mbalimbali lakini zilizompa umaarufu zaidi ni Kaona Mambo Iko Huku na Sanamu la Michelin.

Nasma ambaye pia alipata kuimbia kundi la Babloom Modern ingawa hakung'ara sana, atakumbukwa kutokana na upinzani uliokuwepo miaka ya 1990 kati yake na Khadija Omar Kopa, wakati huo Nasma akiwa Muungano na Khadija akiwa TOT.

Wapenzi wa mipasho wanamkumbuka Nasma ambaye alikuwa akiimba mashairi yaliyotungwa na Mustapha Ramadhan wakiwa Muungano, wakishindana na Kopa aliyekuwa akiimba mashairi yaliyotungwa na Othman Soud wote wakiwa TOT. Ilifikia wakati misemo kama Taarab Imo? Au Taarab Anayo, ilikuwa maarufu nchini na ilitokana na nyimbo za mipasho za Nasma na Kopa.

Akizungumza jana kutoka Biharamulo ambako kundi la TOT Plus lipo kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, Khadija ambaye hujulikana kama Malkia wa mipasho, alisema msiba wa Nasma ni pigo kwa taarabu na ameupokea kwa masikitiko maana alikuwa mtu wake wa karibu.

"Alikuwa kama dada yangu, wengi walidhani sisi ni maadui, lakini ukweli ni kuwa tulikuwa wapinzani jukwaani, lakini nje ya jukwaa ni watu wamoja na wenye kuheshimiana. "Kuna matangazo nilipewa nifanye lakini nikawaambia nikiwa na Nasma itapendeza zaidi, sasa kama ingekuwa nina upinzani naye sidhani kama ningemuunganisha kwenye ile kazi.

"Jambo la msingi tumuombee mwenzetu Mwenyezi Mungu amuweke mahali pema peponi, maana kifo ni cha kila mtu, wote ni waja wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea," alisema Khadija. Nasma pia alipata kushirikishwa na kundi la muziki wa kizazi kipya la Gangwe Mobb lililokuwa likiundwa na Haruna Kahena 'Inspekta Haroun' na Kalama Bakari 'Luteni Kalama' katika wimbo Vidonge. Hadi umauti unamkuta alirekodi na kundi la taarab la Super Shine wimbo uitwao Unajishuku, ambao umekuwa maarufu katika vituo mbalimbali vya redio nchini. Mungu amuweke Mahali Pema Peponi.


..
Online Radio Live
Posted by Dullonet: 22.06.2009
Source: Mwandishi Maalum