LICHA ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuapa kwamba yuko tayari kusulubiwa kuliko kutoboa siri za Kampuni ya Meremeta, bado kauli hiyo haijaeleweka baada ya bunge kuendelea kuhoji sababu za serikali kusita kutoa taarifa za hesabu za kampuni hiyo kwa ajili ya ukaguzi.
Mwaka jana Pinda baada ya kubanwa na wapinzani, alisema kamwe asingeweza kutoboa siri za Meremeta inayojihusisha na uchimbaji wa madini katika mgodi wa dhahabu Buhemba, kwa madai ina uhusiano na usalama wa taifa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ).
Mbali ya Pinda kuapa, jana Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, bado iliendelea kuhoji kuhusu ufisadi wa Meremeta ili kujua ni kwanini serikali inagoma kukabidhi hesabu kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Akisoma taarifa ya kamati hiyo bungeni mjini Dodoma jana Mwenyekiti wa kamati hiyo Zitto Kabwe, alisema Juni 8, mwaka jana bunge lilimwandikia barua CAG ikimtaka akague hesabu za Meremeta ambazo zimegubikwa na utata wa ufisadi.
Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, alisema licha ya kamati kumwandikia CAG akague hesabu hizo, bado hazina ilisita kutoa ushirikiano kwa mkaguzi huyo hadi hivi sasa.
"Juni 8, mwaka 2009 kamati ilimwandikia barua Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali akague hesabu za kampuni Buhemba Gold Mine (Meremeta), na CAG aliomba lakini serikali haijaibu," alifafanua Zitto.
Aliongeza kwamba, kamati yake bado imeshikilia msimamo wa kutaka serikali ipeleke hesabu za kampuni hiyo kwa CAG kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi na kuondoa utata.
Zitto alikuwa akizungumzia utekelezaji wa maagizo ya kamati kwenda kwa serikali katika taarifa ya kamati hiyo ya mwaka 2007/08, ambayo inaonyesha baadhi ya maagizo ikiwemo hilo la kutaka CAG akague hesabu za Meremeta halijatekelezwa.
Agizo hilo pia lilikuwa likitaka uhakiki wa mali na mtaji katika mgodi huo na kwa upande wa serikali usimamizi ufanywe na Shirika la Madini la Taifa (Stamico), kitu ambacho pia hakijafanywa.
Kuhusu Tangold ambayo inatajwa katika mradi huo, Zitto alisema ilibainika kuwa na dola 10 milioni (takriban Sh 15 bilioni) na kusisitiza, bado kunahitajika uwazi.
Akizungumzia agizo la kutaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ijitoe katika kuwa na hisa na kampuni ya Mwananchi Gold yenye tuhuma za ufisadi, alisema anashangazwa kwa kuwa hadi sasa hakuna hatua zilizofanyika.