MENEJA wa Idara ya Madeni ya Nje (EPA) wa benki Kuu ya Tanzania (BoT), Steven Mwakalukwa ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa ulipaji wa zaidi ya Sh 6 bilioni za EPA zinazodaiwa kuibwa na kampuni ya Kernel Ltd, ulikuwa sahihi kwa sababu ulifuata kanuni na taratibu zote za kibenki.
Mwakalukwa ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa mashtaka aliyaeleza hayo jana mbele ya jopo la mahakimu watatu lililokuwa likiongozwa na hakimu Prophil Lyimo.
Katika kesi hiyo, wakurugenzi wa kampuni ya Kernel Ltd, Johnson Lukaza na ndugu yake Mwesiga Lukaza wanadaiwa kuwa Novemba 2, mwaka 2003 jijini Dar es Salaam waligushi hati ya kuhamisha deni kati yake na kampuni ya Marubeni ya nchini Japan.
Shahidi huyo wa upande wa mashtaka alidai kuwa ulipaji wa zaidi ya Sh 6 bilioni kutoka BoT kwenda kwenye akaunti ya kampuni ya Kernel Ltd, ulikuwa sahihi kwa kuwa ulifuata kanuni na taratibu zote za kibenki.
“Malipo kama hayo yanalipwa kwa kufuata kanuni na taratibu za kibenki zilizowekwa na kama yasingeweza kukidhi kanuni na taratibu za kibenki yasingelipwa,” alidai Mwakalukwa baada ya kuulizwa swali na wakili wa utetezi Alex Mgongolwa.
Mgongolwa alitaka kujua endapo ni sahihi malipo yanayotoka BoT kulipwa kiholela.
Awali Mwakalukwa akiongozwa na Wakili wa Serikali, Timon Vitalis alidai kuwa mwaka 2005 alikuwa akifanya kazi katika idara hiyo ya madeni ya nje kama msimamizi wa malipo.
Alieleza kuwa majukumu yake yalikuwa ni kuangalia usahihi na kupokea majalada ya maalipo yanayoingia kwenye idara hiyo na kwamba anaitambua kampuni ya Kernel Ltd kwa sababu aliwahi kuhusika na maalipo ya kampuni hiyo ambayo waliyafanya kwa njia ya mtandao TISS.
Baada ya kutoa ushahidi huo, Vitalis alimuonyesha jalada la BoT la malipo ya kampuni ya Kernel Ltd na shahidi huyo kulitambua akieleza kuwa baadhi ya nyaraka alizisaini yeye.
Jalada hilo ambalo lilipokelewa na mahakama kama moja ya kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo, lilikuwa na nyaraka mbalimbali ikiwepo barua ya Kernel Ltd kwenda BoT ya Novemba 5, 2005 iliyoandikwa na Johnson Lukaza akiomba kulipwa deni hilo la Maruben.
Nyaraka nyingine zilizokuwepo kwenye jalada hilo ni zile zilizokuwa zikionyesha BoT ilikubali kulipa kiasi cha zaidi ya Sh 6 bilioni kwa kampuni ya Kernel Ltd baada ya Gavana kuridhia Desemba Mosi, 2005.
Nyaraka zilizoandikwa na BoT kwenda kwa Kernel Ltd zilieleza kukubaliana na maombi ya kampuni hiyo na kulipwa kiasi hicho cha fedha na kuwa awali malipo hayo yaliidhinishwa na Mkuu wa Idara ya Madeni ya Nje kabla Mkurugenzi wa fedha hajatia saini yake Desemba 6, 2005.
Pia katika jalada hilo kulikuwemo vocha ya malipo ya kampuni ya Kernel Ltd yaliyofanyika Desemba 7 mwaka 2005. Malipo hayo ya zaidi ya Sh 6 bilioni kwenda benki ya BOA ambayo wakati huo ilikuwa ikijulikana kama Euro African, yaliyofanyika kwa njia ya mtandao ambayo Mwakalukwa mwenyewe aliyaidhinisha.
Kesi hiyo inatarajiwa kutolewa ushahidi na watu 14 wa upande wa mashtaka baadhi wakitoka BoT na wengine Wakala wa Usajili wa Makampuni na Majina ya biashara (BRELA) na Jeshi la Polisi.
Katika kesi hiyo, wafanyabiashara hao ambao pia ni wakurugenzi wa kampuni ya Kernel Ltd Johnson Lukaza na ndugu yake Mwesiga Lukaza wanadaiwa kuwa Desemba 3, mwaka 2005 jijini Dar es Salaam walikula njama ya kufanya ubadhirifu wa Sh 6 milioni za BoT.
Pia wanadaiwa kuwa Novemba 2, mwaka 2003 jijini Dar es Salaam waligushi hati ya kuhamisha deni kati ya kampuni yao ya Kernel Ltd na Marubeni ya nchini Japan.
Wanadaiwa kuwa Novemba 14, mwaka 2005 walitoa hati za uongo za uhamishaji deni na Desemba 7, mwaka 2005 walijipatia kwa njia ya udanganyifu Sh 6.3 bilioni ambazo ni mali ya BoT.
Katika hatua nyingine kigogo wa zamani wa BoT, Amatus Liyumba leo anatarajiwa kuanza kutoa utetezi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Aprili 16, mwaka huu Liyumba aliwasilisha orodha ya mashahidi watakaomtetea katika kesi yake hiyo na yeye mwenyewe kupangwa wa kwanza kuanza kutoa utetezi huo.
Wengine watakaomtetea Liyumba katika kesi hiyo ni mshtakiwa wa EPA, Bosco Kimela ambaye aliwahi kuwa Kaimu Katibu na Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi ya BoT, Mkaguzi wa zamani wa Mahesabu wa benki hiyo, Rashid Mwanga na Mkurugenzi wa zamani wa fedha wa BOT, Elisa Isangya.
Kati ya mashahidi hao, Kimela na Elisa awali walikuwa miungoni mwa mashahidi 15 wa upande wa mashtaka waliotarajiwa kutoa ushaidi katika kesi hiyo.
Tayari Liyumba ameanza kupata ahueni katika kesi hiyo baada ya mahakama kumfutia shtaka la kuisababishia serikali hasara ya Sh 221 bilioni katika mradi wa ujenzi wa maghorofa pacha ya BoT Aprili 9,mwaka huu na kubakiwa na shtaka la kutumia madaraka vibaya wakati akiwa mtumishi wa umma katika BoT kati ya mwaka 2001 na 2007.
Kiongozi wa jopo la Mahakimu watatu wanaoisikiliza kesi hiyo, Edson Mkasimongwa alisema alipokuwa analifuta shtaka hili kuwa ili mshtakiwa aweze kuthibika kuwa ni kweli mwajili wake amepata hasara ni lazima mtu anayetuhumiwa kuisababisha awe ameisababisha kwa makusudi au uzembe.
.
.
.
.