AMRI ya kutouzwa kwa nafaka nje kwa ajili ya kujihakikishia usalama wa chakula, itaendelea kuwapo kwa muda pamoja na matarajio ya kuongezeka kwa mavuno mwaka huu, Naibu Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika Dk.David Mathayo alisema bungeni jana.
Dk.Mathayo alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Cynthia Ngoye (CCM) ambaye alitaka kujua kama Serikali itatoa ruksa ya kuuza nafaka hasa baada ya kuongezeka kwa uzalishaji wa mahindi.
Mathayo alisema Serikali kwa sasa inaruhusu mauzo ya mpunga nje kwa kuwa inaonekana wazi kuna kiasi kingi cha mpunga lakini shauri la kuza mahindi litategemea tathmini ya akiba iliyopo.
Alisema mahitaji ni tani milioni 10.6 na ni baada ya tathmini na kujiridhisha kuwa kiasi hicho cha akiba kipo, ndipo Serikali itaangalia namna ya kutoa ruksa ya kuuza nafaka nje.
Pamoja na kuzungumzia kuendelea kuzuia mauzo ya mahindi nje, Mathayo alisema Serikali itaomba fedha zaidi bungeni za kununua mahindi kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa ya Chakula hasa baada ya kuonekana kuwa mavuno mwaka huu yatakuwa mengi.
Alisema watasogeza vituo vya ununuzi wa mahindi katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma karibu zaidi na wakulima.
Kauli hiyo ilitokana na swali la msingi la ununuzi wa chakula cha Ghala la Hifadhi ya Taifa (SGR), lililoulizwa na Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM) aliyetaka kujua kama Serikali itasogeza vituo vya ununuzi wa mahindi hasa kutokana na mwelekeo unaoonesha kuwa kutakuwa na mavuno mengi. Mbunge huyo alitaka pia kujua kama soko la mahindi litafunguliwa mapema.
Dk. Mathayo alisema kwamba Wakala wa Hifadhi ya Chakula anatarajiwa kufungua vituo vya ununuzi mapema Julai mwaka huu na kwamba vituo vukuu vitatu ni Makambako, Songea na Sumbawanga.
Alisema Kanda ya Makambako ina vituo vidogo vyaMakambako, Viwawa, Mlangali, Ludewa na Mundindi. Kanda ya Songea inavituo vidogo vya Songea, Mgazini, Kigonsera, Hanga, Mgalula, Rwanda, Namtumbo na Madaba. Kanda ya Sumbawanga ina vituo vidogo vya Sumbawanga, Laela, Matai, Namanyere na Mtenga.
.