Copyright @ 2010 Dullonet.com. All Right Reserved
WAHAMIAJI haramu 68 ambao ni raia wa Ethiopia wamekamatwa wilayani Handeni mkoani Tanga baada ya kuingia nchini kinyume cha sheria.
Wahamiaji hao haramu walikamatwa katika Kijiji cha Mkaramo na Kwamsisi wakiwa wamejificha porini wakitokea nchini mwao.
Kukamatwa kwa wahamiaji hao kumetokana na wananchi wa kijiji hicho kuwatilia shaka ambapo walitoa taarifa polisi na kufanikisha kukamatwa kwao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Liberatus Sabas, alithibitisha kukamatwa kwa Waethiopia hao walioingia nchini kupitia Bahari ya Hindi katika bandari bubu zilizopo wilayani Pangani.
Kamanda Sabas alisema mara baada ya kuingia wilayani Pangani kwa njia ya boti, walikuwa na lengo la kusafiri kuelekea Dar es Salaam.
Wahamiaji hao tayari wamefikishwa leo mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.