SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), jana lilitoa ratiba ya michuano ya Kombe la Taifa, ‘Kili Taifa Cup 2010’, itakayoanza Mei 8 hadi 29 ikishindanisha timu 24 huku mabingwa watetezi, Ilala ikifungua dimba na Mtwara.
Mabingwa hao watetezi ambao mwaka jana walitwaa ubingwa kwa kuwafunga jirani zao Temeke, wamepangwa katika kituo cha Mtwara chenye timu za Lindi, Ruvuma na wenyeji Mtwara.
Kwa mujibu wa Ofisa Michezo wa TFF, Salum Madadi, timu hizo 24 zimegawanywa kwenye vituo sita kabla ya timu zitakazotinga robo fainali kuhamia jijini Dar es Salaam.
Vituo vya michuabno hiyo, vitakuwa katika mikoa ya Dodoma, Tanga, Iringa, Mwanza, Arusha na Mtwara.
Kituo cha Dodoma, kitakuwa na timu za wenyeji Dodoma, Kigoma, Singida na timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20.
Kituo cha Tanga, kitakuwa na timu za Morogoro, Pwani na Temeke na wenyeji Tanga huku kituo cha Mwanza kikiwa na timu za Kagera, Shinyanga, Tabora na Mwanza.
Madadi alisema, katika kituo cha Arusha, kitakuwa na timu za Mara, Manyara na Kilimanjaro na Arusha wenyewe ‘Meru Warriors’ huku kituo cha Iringa kikiwa na timu za Mbeya, Rukwa, Kinondoni na wenyeji Iringa.
Kituo cha Mtwara, kitakuwa na timu za Lindi, Ruvuma, wenyeji Mtwara na Mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Ilala.
Alisema, hatua ya robo fainali ya michuano hiyo itaanza Mei 23 kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Hatua ya nusu fainali itachezwa Mei 25 huku mshindi wa tatu akitafutwa Mei 28 kabla ya fainali kupigwa
Mei 29.
Madadi alitoa wito kwa timu shiriki kushindana ili wadhamini kuongeza nguvu katika mashindano yajayo.
Naye Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), David Minja, alitoa wito kwa timu shiriki kufika vituoni kwa wakati ili zishiriki ipasavyo mashindano hayo.
Minja alisema timu zionyeshe ushindani ili kuongeza chachu ya mashindano hayo.
.