VILIO au vicheko vitakavyotawala leo katika majiji ya Mwanza na Mbeya baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa wakati timu za Toto African na Prisons zitapotupa karatazao za mwisho za kubaki Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara kwa msimu mwingine.
Mechi nyingi za leo zinachukuliwa kama za kukamilisha ratiba ya ligi kwa timu nyingi isipokuwa kwa Toto African, Prisons na Manyema ambapo ni klabu moja tu inayoweza kujinasua kutoka kwenye janga la kushuka daraja msimu huu baada ya Moro United kuaga mapema.
Maafande wa Prisons na Toto African wote wana jumla ya Pointi 20 kila mmoja huku Manyema Rangers ikiwa juu yao kwa tofauti ya pointi mbili zaidi.
Manyema wenye kibarua kizito dhidi ya Azam watakuwa wakiomba Prisons na Toto zipoteze mechi zao ili ibaki kwenye ligi.
Prisons ikishinda itafikisha pointi 23 na itakuwa mbele ya Manyema yenye pointi 22 na Toto African pointi 20,hivyo Manyema na Toto kuungana na Moro yenye pointi 15 kushuka daraja.
Prisons watakuwa kwenye uwanja wa Sokoine kuikabili Yanga ambao mwishoni mwa wiki walipokea kipigo cha mabao 4-3 kutoka kwa Simba.
Wakati Toto watakuwa ugenini mjini Bukoba kwenye Uwanja wa Kaitaba kuwakabili wenyeji Kagera Sugar wenye pointi 23 ambao matokeo mabaya ya mchezo huo yanaweza kuwashusha daraja.
Endapo timu hizi tatu za mwisho zote zikishinda kwenye michezo yao Toto itafikisha pointi 23 kama Prisons ikishinda, lakini Manyema Rangers watanusurika kushuka daraja kwa kufikisha pointi 25.
Lakini hali hiyo inaweza kuchukua sura mpya kama Toto wataiifunga Kagera Sugar, Manyema wakatoka suluhu na Azam, huku Prisons wakiichapa Yanga mabao mawili timu zote nne za mwisho zitafikisha pointi 23.
Kwa kuwa Toto imeshafunga mabao 23, Manyema 20, Prisons 18 wakati Kagera imeziona nyavu mara 14 tu.
Hapo ndipo Kagera Sugar na Manyema Rangers zitakapoungana na Moro United kushuka daraja kwa kutumia sheria ya mabao mengi ya kushinda katika kuamua.
Kocha wa Prisons, James Nestory amesema bado wana uwezo mkubwa wa kuifunga Yanga na matarajio yao ni kuona wanabaki katika Ligi Kuu.
"Ni kweli tunakabiliwa na mchezo mgumu mbele yetu dhidi ya Yanga, lakini nia yetu ni kuona tunazidi kubaki katika Ligi Kuu msimu ujao hivyo tutahakikisha tunashinda katika mchezo huu ili tusiweze kushuka daraja,"alisema Nestory kwa njia ya simu kutoka Mbeya.
Simba inaingia uwanjani kwa lengo la kukamilisha ratiba huku Mtibwa wakiwa na matumaini ya ushindi ili kuishusha Azam nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 35.
Mtibwa 32, kwa sasa inalingana kwa pointi na Azam wakitofautina na idadi ya mabao ya kushinda, licha ya kutabiri kuwa ni mchezo mgumu kwao bado kocha Mecky Mexime anajipa matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi.
"Simba wao wanacheza mchezo wa kukamilisha ratiba kwani tayari wametwaa ubingwa na sisi tunacheza ili kusaka nafasi ya tatu kwa hiyo kwetu inatupa matumaini zaidi kwani sisi tutakua tukicheza kiushindani zaidi tofauti na Simba ambao wanakamilisha ratiba,"alisema Mexime.
Mbali ya Simba kucheza kwa ajili ya kukamilisha ratiba ya ligi kuu pia mchezo huo utakuwa ni moja ya maandalizi dhidi ya mchezo wao wa Jumapili na timu ya Haras El-Hodood ya Misri kwenye mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika msimamo wa ligi Simba inaongoza kwa pointi59, Yanga 48, Azam 32, Mtibwa 32, JKT Ruvu 24, Afrikan Lyon 24, Majimaji ya Songea24, Kagera sugar 23, Manyema Rangeres 22, Prison 22,Toto African 20 na Moro United15.