Na Asha Bani, Zanzibar
JUMUIYA ya Waendeshaji wa Mashirika ya Utalii ya Zanzibar (ZATO), imesema kwa kipindi cha mwaka jana ilivunja rekodi kwa kupokea wageni wengi kuliko miaka ya nyuma.
Akizungumza hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa ZATO, Munira Saidi, alisema mwaka jana walipokea wageni wapatao 175,000, idadi ambayo ni kubwa kuliko miaka ya nyuma.
Alisema kupanda kwa idadi hiyo kunatokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanza kukua kwa uchumi ambao kwa mwaka 2010 ulikumbwa na mtikisiko.
Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili, alisema wizi umeshika kasi kutokana na watalii wengi kuibiwa vitu vyao, jambo aliloiomba serikali kuongeza ulinzi.
Aidha wameiomba serikali kuweka mabadiliko ya kusikiliza kesi zinazotokana na masuala ya utalii hasa wizi, zimalizike kwa kipindi cha saa 24 kwa kuwa mtalii si mkaaji.
Naye Mwenyekiti wa ZATO, Ally Amour, alisema kuwa kwa sasa wanatumia nguvu katika kushawishi serikali ijitahidi kuitangaza Zanzibar kama kituo cha utalii kulingana na utofauti wake.
Ofisa utawala wa jumuia hiyo, Thabit Abdulazak, aliitaka jamii iwe na mwamko wa kutembelea sehemu mbalimbali za utalii na kushirikiana katika suala la utunzaji wa mazingira katika sehemu za vivutio vya utalii.
Source: Tanzania Daima
