Na Julieth Mkireri, Kibaha
HALMASHAURI za wilaya mkoani Pwani zimetakiwa kuandaa mfumo wa kutoa mafunzo ya lugha ya alama kwa jamii ili wananchi waweze kuwasiliana na watu wenye ulemavu wa kusikia ambao wanapaswa kushirikishwa katika shule mbalimbali za kijamii.
Ushauri huo umetolewa mjini hapa na mtafiti mkuu wa utafiti uliofanywa na mtandao wa wanawake viziwi mkoani, Pwani Tunsime Kyando, wakati akihitimisha utafiti uliofanywa na mtandao huo kwa lengo la kupata takwimu za wanawake viziwi katika wilaya tatu za mkoa huo pamoja na kuibua mahitaji yanayowalenga wanawake hao.
Utafiti huo ambao ulifanyika kwa ufadhili wa shirika la The Foundation For Civil Society umebaini kuwepo kwa changamoto nyingi kwa wanawake viziwi ikiwemo kutojua lugha ya alama na hivyo kushindwa kuwasiliana na jamii inayowazunguka.
Kyando alisema wanawake wengi viziwi wana vipaji lakini wanashindwa kuvitumia kutokana na kukosa wakalimani katika maeneo yao wanayoishi na hivyo kuendelea kuishi katika mazingira magumu ya kimaisha.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi wilaya ya Kibaha Daudi Kulangwa alisema kuwa mtandao wa wanawake viziwi umeundwa baada ya kubainika kuwepo kwa wanawake wengi ambao wanashindwa kupigania haki zao.
Kulangwa alisema kuwa mtandao huo pia umefanya utafiti huo ili kubaini wanawake wengi walio kwenye jamii na hawapati haki zao kama ilivyo kwa watu wengine ambao hawana ulemavu.
Aliwashauri maofisa ustawi wa jamii kuwa na takwimu sahihi za walemavu katika maeneo yao ili wafadhili wanapotokea waweze kuwasaidia kwa urahisi kuliko hali iliyopo sasa kwa maofisa hao ambao wengi wao hawana idadi sahihi ya walemavu walioko kwenye kata na hata wilaya.
Mkoa wa Pwani una viziwi wanawake 300 ambapo utafiti uliofanywa kwenye wilaya za Kisarawe, Mafia na Rufiji umebainisha kuwepo na wanawake wengi ambao hawana elimu na wengi wao wanadaiwa kukatisha masomo kwa kukosa walimu wa lugha ya alama shuleni.
Source: Tanzania Daima
