Wananchi Mwanga wafunga ofisi ya kijiji

Na Rodrick Mushi, Mwanga

WANANCHI wa kijiji cha Kileo, kata ya Kileo, wilayani Mwanga, wamefunga ofisi ya serikali ya kijiji hicho kwa madai ya kuchoshwa na uongozi wao kwa kile kilichodaiwa kushindwa kuitisha mkutano wa kijiji kwa miaka mitatu sasa.

Hatua hiyo ilifikiwa na wananchi hao baada ya kufika eneo hilo kwa ajili ya mkutano uliotakiwa kufanyika Januari 25 mwaka huu lakini muda mfupi baadaye mwenyekiti wao John Rajabu alitangaza kuahirishwa kwake kutokana na kutofika kwa mkurugenzi wa wilaya ya Mwanga, Willy Njau, hali iliyosababisha wananchi kukasirishwa na kitendo hicho.

Hata hivyo walimtaka mwenyekiti huyo kutoahirisha mkutano huo na badala yake kukaa na kujadiliana kuhusu kero zao hizo lakini kabla ya hilo kufanyika wananchi hao walikubaliana kuifunga ofisi hiyo hadi mkurugenzi huyo atakapofika kusikiliza kero zao lakini pamoja na uamuzi huo hakufika.

Bakari Mmbaga alisema anashangazwa na kitendo kilichofanywa pia na baadhi ya wajumbe wa serikali ya kijiji ambao waliondoka muda mfupi baada ya kufika kwenye mkutano huo wakiambatana na ofisa mtendaji wa kijiji.

Naye Philipo Samson alisema kuna shughuli mbalimbali za maendeleo ambazo zimekwama kutokana na kutokuwepo kwa ushirikiano kati ya mwenyekiti na wajumbe wa serikali ya kijiji ambao kwenye mkutano huo walitegemea kufika kwa mkurugenzi huyo.

Miongoni mwa miradi iliyokwama kukamilishwa ni kituo cha afya cha kileo ambacho hadi sasa huduma zake zinasua sua, mradi wa Mkurabita uliokuwepo kwenye kijiji hicho na mifereji ambayo inategemewa na kilimo ambayo haijaboreshwa licha ya msimu wa kilimo kukaribia.

Akizungumzia baadaye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Willy Njau alisema ameyapata malalamiko hayo hivyo wameshaanza kuyachukulia hatua.

Aliahidi pia kufanya kikao Februari 8 ili kujadilili changamoto zinazowakabili wananchi.

Source: Tanzania Daima

About Dullonet