John Semnkande, Pangani, Frederick Katulanda, Mwanza
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi wanaivuruga CCM na kumtaka Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete kuwang’oa ili kulinda heshima ya chama hicho kinachotawala .
Lakini wakati Sumaye akitaka mafisadi wafukuzwe, Rais Kikwete kwa upande wake, alirejea agizo la Nec la Aprili mwaka jana la kuwataka wote wanaokichafua chama, wawajibishwe na kwamba, chama hakiwezi kuacha kutekeleza matakwa ya wengi kwa kuhofia kuwaudhi wachache.
Mpango Mkakati wa CCM kujihuisha kwa kujivua gamba uliotangazwa na mwenyekiti wake katika maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa chama hicho yaliyofanyika mjini Dodoma mwaka jana, lakini hadi sasa mpango huo haujatekelezwa na kurudishwa katika Kamati Kuu (CC).
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa chama hicho yaliyofanyika Pangani mkaoni Tanga, Sumaye alimshauri Rais Kikwete kuwafukuza watuhumiwa hao kama hawatajiondoa wenyewe ili kulinda heshima ya chama hicho.
“Hatuwezi kuwa na chama imara kama hatukuondoa magamba, mwenyekiti wetu wa chama taifa lazima tuyaondoe magamba yanayokipaka chama matope.” alisisitiza.
Alisema CCM inaelekea kwenye kipindi cha uchaguzi wa ndani ya chama na kwa msingi huo kinapaswa kuondoa mabaya yaliyojitokeza na kujiwekea misingi imara kwa kuwaondoa viongozi mafisadi na wala rushwa.
Alisema CCM ni chama chenye misingi imara lakini, baadhi ya watu ndani ya chama hicho wameanza kukiharibu kwa kutoa rushwa wakati wa uchaguzi wa ndani na hata wa Serikali, jambo linalowafanya wanachama kujenga dhana kwamba, kipindi cha uchaguzi ni cha mavuno.
Sumaye alisema ni vema sasa hatua zikachukuliwa kuziba mashimo kwa kuwakataa viongozi wanaoomba nafasi mbalimbali kwa kutoa rushwa au kuwekwa na watu fulani ili kulinda maslahi yao.
Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM, aliongeza kwamba inapofika kipindi cha uchaguzi baadhi ya wagombea wamekuwa na tabia ya kuuza vitu vyao kwa lengo la kujipatia fedha za kuwanunua wapiga kura, jambo ambalo alisema si zuri .
Alitumia nafasi hiyo kwa kuwataka viongozi wa chama hicho, kuacha tabia ya kuchafuana na kunyoosheana vidole na badala yake, wafuate misingi ya kazi ili kukiwezesha chama kufikia malengo.
“Watu wanafikiria kutoa rushwa ni kukijenga chama, kumbe wanakibomoa na kukisababisha malalamiko,matatizo pamoja na kukosa ufanisi katika utekelezaji,”alisema Sumaye.
Pia aliwataka viongozi na wanachama wa kuacha tabia ya kujenga makundi ya kuchafuana na kutumia magazeti.
Alisema katika uchaguzi unaokuja ndani ya CCM, chama kinataka kipate viongozi ambao hawatatumia vishawishi vya rushwa au kuwekwa na mtu fulani.
Sumaye alibainisha kuwa lengo kubwa ni kuwapata viongozi wanaofaa na wenye moyo wa kutumikia wananchi.
“Baadhi ya viongozi wa CCM wamepotoka na kama hawakubali watakuwa wanajidanganya wenyewe, pamoja na mazuri mengi yaliofanywa na chama hicho yapo machache yanayokichafua chama yanayofanywa na viongozi hao wasiokitakia mema,”alisema.
JK: Lazima wang’oke
Akihutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jiini Mwanza jana, Rais Kikwete alirejea msimamo na maazimio ya Nec wa kutaka kusafisha chama.
Rais Kikwete alisema Nec hiyo ya Aprili mwaka jana ilitoa maazimio 23 ambayo moja ni hilo la chama kujihusisha na kuongeza kwamba, chama hicho bado kinakubalika miongoni mwa wa Watanzania lakini, wapo baadhi ya watu wachache wanaokipotezea mvuto.
, “Hao wanaodhani uamuzi huu wa kukihuisha chama ni wa hovyo, basi wao ndiyo wa hovyo. Uamuzi huu lazima utekelezwe, hatuwezi kuacha kutekeleza matakwa ya wengi ili kuwafurahisha wachache,” alisema
Rais Kikwete alisema watu wachache wasiokuwa na maadili lazima washughulikiwe huku akitaka kuimarishwa kwa Kamati za Maadili na Usalama za chama hicho kuanzia ngazi za chini hadi taifa, ili kuhakikisha kuwa chama kinabaki na watu safi .
Alisema hakuna mtu aliyebora zaidi ya CCM na kurejea kauli ya Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Benjamin Mkapa, ambaye alikuwa akisisitiza, “chama kwanza mtu baadaye.”
Alisema ndani ya CCM wazalendo, wachochezi, watu wanaotaka umoja na mshikamano wanajulikana kwa kauli na matendo yao.
“Wapo ambao wanaojiita wana CCM lakini leo utawasikia wametoa kauli huko mara kule. Lakini, hawa tutakuja kuwakumbusha siku moja.”
Uchaguzi wa ndani
Mwenyekiti huyo wa CCM, alisema uchaguzi ndani ya chama ni muhimu kwa sababu viongozi watakaopatikana ndiyo watakaosimamia chama kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Alisema kwa msingi huo ni vema wanaCCM wakatambua umuhimu wa kupata viongozi bora ambao hawatatokana na fedha.
Aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukurua), kukaa tayari kuwashughulikia wote watakaobainika kutoa na kupokea rushwa katika uchaguzi huo.
Rais Kikwete alisema Takukuru inapaswa kutumia sheria ya gharama za uchaguzi kuwashughulikia wale watakaotumia fedha katika kutafua madaraka kupitia uchaguzi huo.
Hali kadhalika ale watakaopokea ili kuchagua wagombea.
“Na ninyi msikubali kununuliwa kwa shilingi 1,000. Hivi mtu kweli unauza utu wako kwa shilingi 1,000 Siku moja, ndugu yangu marehemu Ditopile (Mzuzuri), aliwahi kuulizwa na wakazi wa Dar es Salaam kipindi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwamba, wewe unataka kugombea Ubunge, je shida zetu unazijua,” alisema na kuongeza,
“Akawajibu ndiyo, tatizo lenu ni ulofa. Yaani watu wazima wake wenye waume zenu na waume wenye wake zenu mnakubali kufungiwa gesti na kupewa Sh2,000i na kipapatio cha kuku, kama si ulofa ni nini, Sasa na ninyi msikubali kununuliwa,” alisema.
Source: Mwananchi
