NSSF kuuza hisa kwa wanachama

Na Grace Macha, Arusha

WADAU wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), wameuagiza uongozi wa mfuko huo kuanzisha mipango na mchakato wa kuuza hisa kwa wanachama wake katika miradi mikubwa ya kiuchumi inayowekeza ili kuongeza pato la wanachama na wastaafu.

Hiyo ni miongoni mwa maazimio yaliyoafikiwa baada ya mkutano wao wa siku tatu uliofanyika jijini Arusha na kumalizika mwishoni mwa wiki.

Mwenyekiti wa bodi ya udhibiti wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini (SSRA), Siraju Kaboyonga, akizungumzia suala hilo alishauri michango ya wanachama itumike kununulia hisa hizo pindi mpango huo utakapoanza kutekelezwa badala ya kuwataka kutoa fedha taslimu mifukoni.

“Tukisema wanachama watoe fedha taslimu kutoka mifukoni mwao kununua hisa itakuwa ni sawa na kuwanyima fursa hiyo kwa sababu wengi hawatamudu kutokana na hali halisi ya mishahara na vipato vyao,” alisema Kaboyonga.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhan Dau, alikubaliana na hoja hiyo akisema busara ya kawaida inaelekeza kuwa fedha za michango ya wanachama ndizo zitumike kununulia hisa, ingawa hakutaka kuzungumzia suala hilo kiundani.

Hata hivyo, Dk. Dau alibainisha kuwa katika kutekeleza mpango huo, shirika
litatenga asilimia maalumu ya hisa kwa ajili ya kuuzwa kwa wanachama pekee na kiasi kinachosalia kitauzwa kwa umma kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudancia Kabaka, alisema tayari muswada wa sheria kufanikisha malengo hayo umewasilishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma.

Waziri Kabaka alisema wataalamu kutoka wizarani na idara nyingine serikalini wametembelea nchi jirani ya Kenya kujifunza uendeshaji na utekelezaji wa mpango wa ‘pensheni’ kwa wazee.

Source: Tanzania Daima

About Dullonet