‘Majengo yasiyofaa yameathiri utendaji wa serikali’

Na Happiness Mtweve, Dodoma

IMEELEZWA kuwa utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za serikali katika majengo yasiyofaa na hatari umeathiri kwa kiasi kikubwa utendaji wa serikali katika kuwahudumia wananchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, alisema hayo wakati akizindua jengo la kumbukumbu na nyaraka za taifa lililojengwa katika eneo la kisasa nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Alisema hali hiyo pia imesababisha ucheleweshaji wa kulipwa pensheni kwa watumishi wa umma, ugawaji holela wa viwanja na ucheleweshaji wa kusikiliza kesi, rushwa na upotevu wa mali za umma.

Alisema kutokana na umuhimu wa kuhifadhi kumbukumbu mbalimbali ikiwemo za taifa kuna ulazima wa kujenga majengo yanayofaa na yanayokwenda na wakati ikizingatiwa kwamba hivi sasa dunia imepiga hatua katika suala zima la tekinolojia ya mawasiliano.

Kwa mujibu wa waziri huyo serikali imeuona umuhimu huo na ndiyo maana imeamua kujenga majengo yenye hadhi likiwamo alilolizindua.

Alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo mkoani hapa ni utekelezaji wa azma ya serikali ya kuhamishia ofisi zake mkoani Dodoma ambako ndiko makao makuu ya nchi.

Alisema ujenzi wa kituo hicho umezingatia uzalishaji wa taarifa za serikali katika teknolojia ya habari na Mawasiliano (Tehama) huku akisema kuwa kituo hicho kitaunganishwa na mtandao wa Serikali Mtandao.

Aidha alisema matumizi ya mtandao huo yatarahisisha upatikanaji wa taarifa na nakala za kumbukumbu zitakazokuwa zinahitajika na watumiaji mbalimbali.

Waziri Ghasia alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha watendaji wakuu wa ofisi mbalimbali za umma kuhusu wajibu wao wa kutunza kumbukumbu zinazozalishwa katika ofisi zao kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa na mamlaka husika ili kituo hicho kiweze kupokea na kutunza kumbukumbu ipasavyo.

Source: Tanzania Daima

About Dullonet