Kamati ya bunge yaanza kuzungumza na madaktari

Geofrey Nyang’oro na Keneth Goliama
KAMATI ya Bunge ya Huduma za Jamii, leo inaanza rasmi kazi ya kusuluhisha mgogoro wa madaktari na serikali uliowafanya wanatalaama hao kuitisha mgomo nchini nzima.

Bunge limeamua kuingilia kati mgogoro huo baada ya jitihada za Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuumaliza kushindikana na madaktari hao kuendelea na mgomo kwa kipindi cha wiki mbili sasa.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa kikao hicho kitafanyika leo jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa kamati ya madaktari hao Dk Stephen Ulimboka alilithibitishia gazeti hili uwepo wa mkutano huo akieleza kuwa ni muhimu katika kufikia mwafaka wa mgogoro huo ulioanza kuleta athari kubwa kwa jamii.

“Sisi tumepata taarifa za wito kutoka kwa kamati ya bunge na wametueleza kuwa tungekutana nao kesho (leo). Tupo tayari kukutana nao na tunaamini kuwa sasa ukweli kuhusu madai yetu utafahamika, tutawaeleza ukweli na utafika bungeni na kujulikana kwa umma,” alisema Dk Ulimboka.

Alisema jumuiya yao  imejiandaa kukutana na Kamati ya Bunge na kwamba tangu kupata taarifa hizo wamekuwa wakiwasiliana na wenzao walioko mikoani kurudi Dar es Salaam ili kuungana nao kwenye kikao hicho.

Kuhusu mgomo, Dk Ulimboka alisema bado unaendelea hadi hapo watakapoona kuwa madai yao yanasikilizwa na kutekelezwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

“Hapa tulipofikia hatuwezi kurudi nyuma kwa maneno matupu hadi hapo tutakapoona mafanikio ya madai yetu  yameonekana. Lakini sisi ni binadamu, tutaangalia nini tunaweza kufanya katika hilo kwa sababu hata sasa tumeendelea kutoa  huduma za dharura,” alisema.

Kitendo cha Kamati ya Bunge kukutana na madaktari hao kimetajwa kuwa hatua muhimu ya kumaliza mgogoro huo  ambao umeingia siku ya 14 leo ukidhoofisha huduma za tiba katika hospitali kubwa za rufaa nchini.

Madai ya madaktari

Madaktari hao wameitaka serikali kuwalipa posho ikiwamo za kulala kazini walizodai tangu mwaka 2004 hazijawahi kubadilika kutoka kiwango cha sasa cha Sh 10,000 licha ya  mwongozo wa serikali kuelekeza walipwe kwa nusu ya fedha ya mkoa husika.

Pia madaktari hao wamependekeza kulipwa posho kwa wale wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi ili iwatie morali wale wanafanyakazi katika mazingira ya hatarini yanayoweza kuwaambukiza magonjwa na kuwasababisha athari mbalimbali.

Madai mengine ya madaktari hao ni kulipwa posho ya kufanya kazi katika maingira magumu,kupata posho kwa ajiri ya usafiri au mkopo wa gari,kupatiwa nyumba za kuishi,kuboreshewa mishahara yao na kupatiwa bima ya afya wao na familia zao.

Madaktari hao pia walipendekeza waziri Mkuu Mizengo Pinda amshauri Rais Jakaya Kikwete aifumue wizara ya afya na Ustawi wa jamii kwa kuwaondoa kazini Waziri wa afya na Ustawi wa Jamii Dk Hadji Mponda,Naibu wake Dk Lucy Nkya,katibu Mkuu Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa serikali Dk Deo Mtasiwa kwa madai kuwa wameshindwa kutekeleza majukumu yao katika wizara hiyo.

Hali halisi MNH na MOI

Tangu kuanza kwa mgomo hali ya upatikanaji wa tiba katika Hospitali ya taifa ya muhimbili(MNH) na Kitengo cha Tiba ya Mifupa(MOI) ni mbaya na kutokana hali hiyo uongozi wa MOI ulilazimika kusitisha huduma zote za kiliniki kwa wagonjwa.

Wakati huduma MOI zikifungwa MNH nako zimezorata hususani kwa kitengo kinachohudumia wagionjwa wa nje (OPD).
Eneo lingine lililoathirika kwa upenda wa MNH ni kitengo cha huduma za dhararu ambacho kwa sasa kinawatumia madaktari kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Meneja katika kitengo hicho, Optatus Silanda alisema huduma bado zinasuasua kutokana na idadi ndogo ya madaktari wanaofanyakazi katika kitengo hicho.

“Kwa wakati mmoja kitengo hiki huwa na madaktari 15, lakini idadi iliyopo haitoshi kwani kama wagonjwa watafika kwa kiwango cha awali hali itakuwa ngumu,”alisema Silanda.

Katika kitengo hicho kwa sasa kina madaktari 15 kutoka JWTZ na kwamba kimekuwa kikipokea idadi ndogo ya wagonwa hali ambayo imekuwa inatoa unafuu kwa watoa tiba kwa mjibu wa meneja huyo.

Bakwata waomba madaktari

Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) limewaomba madaktari  kurejea  kazini ili kuokoa roho za wanyonge wasio na hatia, huku wakiitaka serikali kufanya mazungumzo haraka.

Tamko hilo lilitolewa jana wakati wa kusherekea siku ya Kuzaliwa kwa Mtume (Maulid) iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja na  Sheikk Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Alhad Mussa Salumu.

Sheikh Salumu  katika kamko hilo waliitaka serikali kufanya haraka mazungumzo  na madaktari ili waweze kurejea kazini.

Sheikh Salumu alisema  Bakwata inatambua  michango  mkubwa wa madakatari katika taifa  wa kuokoa roho za watu na kwamba nafasi hizo zitumiwe kwa kadri mungu alivyowapa.

“Tunaomba  Madakatari rudini kazini wakati  serikali inafanya mazungumzo nanyi tumieni busara kuhakikisha mnaponya roho za watu,” alisema  na kuongeza;

“Serikali inatakiwa kufanya mazungumzo haraka na madaktari kutokana na hali ya watu wasio na hatia wanapoteza maisha” alisema.

Sheikh Salumu alisema jambo hili linahudhunisha  kwa kiasi kikubwa kutokana na kusababisha  madhara ma kubwa kwa taifa huku watu wakipoteza  maisha  na kwamba Serikali isipofanya haraka kufanya mazungumzo na madaktari watu wataendeleza kupoteza maisha ili hali serikali ipo .

Source: Mwananchi

About Dullonet