Watu binafsi waliouziwa nyumba hizo kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Ester Chilambo ambaye aliuziwa nyumba kwa thamani ya Sh milioni 21.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakati wa kuuzwa kwa nyumba hiyo alikuwa mtumishi wa Mipango, lakini wakati wa kusaini mkataba alikuwa amehamia Radio Tumaini, haikufafanuliwa kama nyumba hiyo inarudishwa serikalini au ataendelea kuwa nayo. Mwingine ni Mussa Joseph ambaye aliuziwa nyumba iliyopo Ubungo Camp kwa thamani ya Sh milioni 1.5.
Hata hivyo, mteja huyo wa serikali alipokabidhiwa barua ya kusitisha mkataba, alifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania na hata aliposhindwa kesi, alikata rufaa na shauri lake liko mahakamani bado. Pia yumo Stanley Manongi, ambaye aliuziwa nyumba iliyopo Ubungo Camp kwa Sh milioni 13 ambaye amesharejeshewa fedha zake na nyumba hiyo amepewa mtumishi mwingine wa umma.
Wa mwisho katika kundi la watu binafsi waliouziwa nyumba za serikali ni Monica Senga, ambaye aliuziwa nyumba iliyopo Charambe Upanga kwa Sh milioni 14. Hata hivyo pamoja na mteja huyo kukubali kufutiwa mkataba, serikali imependekeza apangishwe katika nyumba hiyo kibiashara, kwa vile ameifanyia matengenezo makubwa hivyo bado anaishi katika nyumba hiyo.
Taarifa hiyo pia iliwataja watumishi waliouziwa nyumba zaidi ya moja kinyume na utaratibu, akiwamo Dk. Edna Moses, Veronica Mabula, Switbert Bajuza na Agnes Chamshama. Pia ilitaja majina ya watu ambao katika familia moja walinunua nyumba mbili au zaidi. Familia hizo ni ya Ben na Dk. Edna Moses, familia ya Hussein Abdulrahman na Mwanamtama Marandu ya Emil Kayega na Emerensiana Kayega na ya Clement na Esther Mshana.
Familia nyingine ni ya Dk. Jacob na Theodora Mollel na ya Ngore na Zainab Kondo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyumba nyingine zilizouzwa kinyume na utaratibu ni pamoja na zilizoko kwenye kambi za Jeshi. Nyingine ni nyumba za taasisi, zilizouzwa kwa watumishi wa Serikali Kuu na ambazo zilikuwa katika maeneo nyeti ya Serikali ambazo ziliuzwa kwa watumishi wa Serikali.
Taarifa hiyo ambayo ilitaja majina ya kila aliyenunua, ilifafanua kuwa baadhi zilirudishwa na baadhi hazijarudishwa kutokana na kuwa na kesi mahakamani. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika makadirio ya matumizi ya Wizara ya Miundombinu ambayo ilisitishwa kuhitimishwa jana kutokana na mahitaji ya kuifanyia mabadiliko makubwa, kulikuwa na Sh bilioni 1.5 zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia za nyumba zitakazorudishwa serikalini.
.